Thursday, November 22, 2012

Kinana atangaza vita viwanda vya korosho

“Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi ama virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii, nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ametangaza vita dhidi ya vigogo walionunua viwanda vya kubangua korosho, lakini wakashindwa kuviendeleza na akaitaka Serikali iwanyang’anye.
Amesema vigogo hao ambao walinunua viwanda 12 vya kubangua korosho vya Serikali hivi sasa havifanyi kazi na vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia mazao. Kinana alisema hayo jana mkoani Mtwara wakati akiwahutubia wanachama wa tawi la CCM katika Kijiji cha Mkunwa kilichopo katika Wilaya ya Mtwara. “Wamenunua viwanda vyetu, lakini wameshindwa kuviendeleza, ajira zimepotea, wananchi wa Mtwara wanaendelea kuwa maskini,” alisema Kinana. Alisema wakati viwanda hivyo vikifanya kazi, kila kimoja kiliweza kuajiri watu wengi, lakini sasa hivi vijana wanakosa kazi kwa sababu viwanda hivyo vimefungwa. “Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi ama virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii, nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” alisema Kinana. Alisema maghala ya viwanda hivyo hivi sasa yanahifadhi korosho ambazo hazijabanguliwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Uchina na India. “Korosho zinasafirishwa na vigogo hao kwenda nje ya nchi zikiwa hazijabanguliwa, matokeo yake wakulima wanapata fedha kidogo kwa sababu wao hawabangui korosho bali zinakwenda kubanguliwa nje ya nchi,” alisema Kinana. Alisema vigogo hao ndio waliovuruga uchumi wa mikoa ya Kusini kwa sababu ajira zilizokuwa zikipatikana zamani hivi sasa hazipo kwa sababu wameua viwanda walivyokabidhiwa. Alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakitumia viwanda hivyo kuombea mikopo kwenye benki ili kuendeleza biashara ya korosho ambayo inamnyonya mkulima na kuwafaidisha wao. “Tumechoka, sasa ni lazima tukatae unyonyaji huu. Wabunge wa Mtwara ni lazima tusaidiane kulisimamia hili hata kama kwa kutunga sheria itakayovilinda viwanda vyetu,” alisema. Aliongeza: “Kama wao wamenunua viwanda wakakiuka masharti yanayowataka kuviendeleza, sisi tutashindwa vipi kutunga sheria itakayowalinda wakulima na viwanda vyetu?” alihoji Kinana. Akizungumzia zaidi zao hilo, Kinana alisema wanaofaidika nalo siyo wakulima bali wafanyabiashara na wajanja wachache ambao sasa wamesababisha malalamiko kuendelea kila mwaka. Kinana alisema hayo baada ya wananchi wengi kumlalamikia kwamba walikuwa hawajapata malipo ya korosho zilizokopwa na vyama vya ushirika. “Nashukuru Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza ataendelea kubaki hapa Mtwara ili kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya wakulima wa Korosho,” alisema. Awabana viongozi CCM Akizungumzia uhai wa chama hicho, Kinana alisema kuanzia sasa yeye na viongozi wenzake watakuwa wakitembelea matawi na mashina ya chama hicho kwa sababu huko ndiko kwa wenye chama. “Tulijisahau kidogo huko nyuma, tukawa tunafanya mikutano kwenye mikoa, lakini sasa kila kiongozi wa chama anatakiwa kwenda kwenye mashina na matawi ili kufahamu matatizo ya wanachama,” alisema Kinana. Kinana aliahidi kutoa mifuko ya saruji 100 , mabati na mbao kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ili wanakijiji wa Mkunwa waweze kupata huduma za afya. Kwa upande wake, Chiza ambaye yuko katika ziara hiyo, alisema ataendelea kubaki katika mkoa wa Mtwara na Lindi ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wakulima wa korosho an alisema “Nikiwa katika mikoa hii nitakutana na wenye benki ili kuzungumza nao namna tunavyoweza kupata fedha za wakulima wa korosho”. Awali wakulima wa korosho wa kijiji hicho wakizungumza mbele ya viongozi hao walisema licha ya kuuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani bado hawajalipwa fedha zao. “Tumeuza korosho, lakini ni muda mrefu hatujapata awamu ya pili ya fedha zetu, tunaomba chama kitusaidie,” alisema Hadija Hassan ambaye aliungwa mkono na wanakijiji wengine ambao walisema hiyo ndiyo kero yao kubwa. Akijibu hoja hiyo, Kaimu Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Mtwara, Lilanga Mohamed alisema “Tumekuwa tukifuatilia benki na tumeahidiwa kwamba wiki ijayo fedha hizo zitapatikana na wakulima wataanza kulipwa,” alisema Lilanga.

No comments:

Post a Comment