Tuesday, November 27, 2012

Aibu Yawakumba Mawaziri Mtwara

MAWAZIRI watatu wa Rais Jakaya Kikwete juzi walizomewa baada ya kupanda jukwaani kujibu kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa kwanza wa viongozi wapya wa CCM taifa, ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana. Tukio hilo lilitokea juzi mkoani Mtwara ambako Kinana na mawaziri hao walikuwa katika ziara ya chama kujibu kero mbalimbali za wananchi.Mawaziri waliokumbwa na dhahama hiyo ni Christopher Chiza wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Hawa Ghasia (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi) Naibu wake, Aggrey Mwanri. Chiza ndio alikuwa wa kwanza kukumbana na zomeazomea hiyo, lakini mambo yalikuwa magumu zaidi kwa Ghasia ambaye alizomewa tangu alipoanza kuzungumza mpaka alipomaliza.Ghasia ambaye pia ni mbunge wa Mtwara Vijijini, alirushiwa makombora na Rukia Ismail Athumani ambaye alimshutumu yeye pamoja na Mbunge wa Mtwara mjini, Asnein Murji kwamba waliruhusu gesi kupelekwa Dar es Salaam wakati wananchi wa mkoa huo hawajafaidika nayo. “Ghasia na Murji kwanini mnaudanganya umma kwa kupeleka gesi Dar es Salaam, sisi hatuna ubaya na chama ila hatutaki gesi iende huko” alisema Athumani huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.Kabla ya dada huyo kuteka hisia za wananchi kwa kuwasilisha kero hiyo, Kinana alimruhusu mwananchi mwingine, Issa Kambona ambaye pia alieleza kuwa hakubaliani na suala la gesi hiyo kupelekwa Dar es Salaam. Kinana alisema amesikia hoja hizo za wananchi na kwamba atamueleza Waziri wa Nishati na Madini azungumze na wananchi wa Mtwara kuhusu gesi hiyo.Baada ya mambo kuzidi kuwa magumu, Ghasia alilazimika kupanda jukwaani kujibu makombora aliyokuwa akirushiwa na wananchi waliofika katika mkutano huo. “Sio kweli kwamba hatutetei maslahi yenu, gesi iliyopo ni nyingi hamuwezi kuitumia na kuimaliza, kuna futi za ujazo trilioni 20,000 na tunaweza kuitumia kwa zaidi ya miaka 90, hata hivyo, Wizara ya Nishati na Madini imetoa ofa ya kuwalipia chuo vijana 150 kila mwaka,” alisema Ghasia, lakini wananchi hao waliendelea kumzomea.“Uongo, uongo, hatutaki, hatutaki, huyoo, huyooo” walisikika wakisema wananchi hao, hali iliyomfanya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kuingilia kati, kujaribu kuwatuliza. “Kelele unazozisikia dada (Ghasia) zinaashiria kuna jambo, nafasi hizo 150 hawazipati, kama zinatolewa basi kwa upendeleo,” alisema Nape huku akishangiliwa na wananchi hao.Baada ya hali kutulia kiasi, Ghasia alijaribu kuendelea kutoa ufafanuzi, lakini kitendo cha kuanza kuzungumza, wananchi hao walianza tena kuzomea. “Kila mtu amelelewa katika mazingira tofauti, hilo halinihusu…watu wangu wa Mtwara vijijini wamenielewa,” alisema Ghasia na kuteremka jukwaani hali iliyozidisha kelele za kumzomea.Nape alisawazisha mambo kwa kusema, hoja ya wananchi hao imechukuliwa na itawasilishwa kwa Serikali ili kuona namna ambavyo inaweza kukaa na wananchi hao na kuweka maslahi yao mbele. Ilivyoanza Panzia la zomea zomea lilifunguliwa na Chiza alipopanda jukwaani kujibu hoja ya kuyumba kwa soko la zao la korosho, ambapo wananchi walimpinga baadhi ya kauli alizozitoa.“Tatizo la korosho ni baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika na wengine ni watendaji wa Serikali …nipo hapa na wala siondoki, nitalishughulikia hili ili korosho zinunuliwe” alisema Chiza huku sauti za wananchi zikimpinga kwa kusema “uongooo”. Hata hivyo, Chiza aliweza kukabiliana na hali ya zomeazomea jukwaani baada ya watuliza wananchi kwa kusisitiza kuwa ataendelea kuwapo Mtwara, kushughulikia tatizo hilo ili ununuzi uendelee.Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwanri alipata wakati mgumu mara alipopanda jukwaani na kuanza kuzungumzia namna ya kumaliza kero ndogondogo zinazoletwa na mamlaka zake, wananchi walikuwa wanazoea “huyoo…hatutaki” lakini baada ya kuanza kuongea alionekana kuiteka hadhira na mambo yakawa shwari. “ “Tumesema wauza vitumbua, wasibughudhiwe … mkurugenzi njoo jukwani, nakuagiza kuanzia leo marufuku wanafunzi kurudishwa shuleni kwa sababu ya michango” alisema Mwanri huku akishangiliwa.Awali Kinana alisema mkutano huo unalenga kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi ambazo zinawezakuwa kikwazo kwa chama hicho kuingia madarakani mwaka 2015. Katibu mkuu huyo wa chama tawala alisema umefika wakati wa chama kusimamia utendaji wa Serikali kutatua kero za wananchi wa mkoa wa Mtwara ikiwa ni pamoja na kuyumba kwa soko la korosho na gesi.“Najua hapa kuna kero kubwa mbili, korosho na gesi, nimekuja na Mawaziri hapa watatoa majibu leo” alisema Kinana huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu ulioudhuria mkutano huo. Chanzo: Mwananchi Newspaper, Nov 2012

No comments:

Post a Comment