Friday, December 21, 2012

Salamu za Krismasi na Mwaka Mpya

Ndugu wanakusini, Taasisi yako ya maendeleo ya mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara (South Eastern Development Org - SEDO) inapenda kuwatakia kheri na afya kipindi cha sikukuu na kumaliza mwaka 2012. Pia tunawaombea wote tuvuke salama mwaka huu na kuuanza mwaka 2013 kwa Neema za Mwenyezi Mungu mwenyewe. SEDO inapenda kuwakumbusha slogan yake "Thamani ya mtu ni KUJENGA na KUENDELEZA kwao". Kwa hili tungependa tuanze mwaka 2013 kwa kila mmoja wetu kujichunguza ili kuona ana faida gani kwa jamii ya watu wake kule kusini, lipi umefanya la kuchangia maendeleo ya wasiojiweza, lipi unaweza kulifanya mwaka 2013 kuboresha au kuongeza juhudi kuliboresha na nini ambacho kipo mabegani mwako ambacho kina manufaa kwa wananchi maskini wa Lindi na Mtwara. Tukumbuke juhudi ya mtu mmoja mmoja ni muhimu ila ina tija ndogo kuliko kuunganisha nguvu. Hivyo, wanakusini mnaombwa mwaka 2013 tuutumie kujitazama na kuunganisha nguvu zetu ili kwa pamoja tushinde magumu yanayowakabili ndugu zetu na sisi wenyewe hasa kwenye matatizo ya Elimu, Afya, Soko la korosho na ufuta, mipango ya matumizi ya gesi asilia na migogoro ya ya viongozi ambayo haina tija kwa wananchi maskini. Imetolewa na Uongozi; South Eastern Development Organization - SEDO Ofisi ya Sekretarieti DAR ES SALAAM

Wednesday, December 19, 2012

Job cum business opportunity for Agronomists

Ndugu zangu, Kampuni ya Ujerumani imeniomba nimtafute mtaalamu wa kilimo (yaani Agronomist) mwenye kuanzia shahada ya kilimo ambaye anafanya shughuli zake kibiashara, kajiajiri na yuko dynamic enough ili awe kuwa mwakilishi wao hapa Tanzania kwenye biashara na huduma ya tiba za mimea na kilimo kwa ujumla. Ofisi za kanda ziko Addis Ababa, Ethiopia na nyingine Nairobi, Kenya. Age limit ni below 45 years. Kwa yeyote mwenye sifa hizo au ambaye anamjua mtu mwenye sifa hizi naomba atume CV yake mapema iwezekanavyo kwa E-mail: geoffrey.mwambe@gmail.com

Tuesday, November 27, 2012

Aibu Yawakumba Mawaziri Mtwara

MAWAZIRI watatu wa Rais Jakaya Kikwete juzi walizomewa baada ya kupanda jukwaani kujibu kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa kwanza wa viongozi wapya wa CCM taifa, ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana. Tukio hilo lilitokea juzi mkoani Mtwara ambako Kinana na mawaziri hao walikuwa katika ziara ya chama kujibu kero mbalimbali za wananchi.Mawaziri waliokumbwa na dhahama hiyo ni Christopher Chiza wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Hawa Ghasia (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi) Naibu wake, Aggrey Mwanri. Chiza ndio alikuwa wa kwanza kukumbana na zomeazomea hiyo, lakini mambo yalikuwa magumu zaidi kwa Ghasia ambaye alizomewa tangu alipoanza kuzungumza mpaka alipomaliza.Ghasia ambaye pia ni mbunge wa Mtwara Vijijini, alirushiwa makombora na Rukia Ismail Athumani ambaye alimshutumu yeye pamoja na Mbunge wa Mtwara mjini, Asnein Murji kwamba waliruhusu gesi kupelekwa Dar es Salaam wakati wananchi wa mkoa huo hawajafaidika nayo. “Ghasia na Murji kwanini mnaudanganya umma kwa kupeleka gesi Dar es Salaam, sisi hatuna ubaya na chama ila hatutaki gesi iende huko” alisema Athumani huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.Kabla ya dada huyo kuteka hisia za wananchi kwa kuwasilisha kero hiyo, Kinana alimruhusu mwananchi mwingine, Issa Kambona ambaye pia alieleza kuwa hakubaliani na suala la gesi hiyo kupelekwa Dar es Salaam. Kinana alisema amesikia hoja hizo za wananchi na kwamba atamueleza Waziri wa Nishati na Madini azungumze na wananchi wa Mtwara kuhusu gesi hiyo.Baada ya mambo kuzidi kuwa magumu, Ghasia alilazimika kupanda jukwaani kujibu makombora aliyokuwa akirushiwa na wananchi waliofika katika mkutano huo. “Sio kweli kwamba hatutetei maslahi yenu, gesi iliyopo ni nyingi hamuwezi kuitumia na kuimaliza, kuna futi za ujazo trilioni 20,000 na tunaweza kuitumia kwa zaidi ya miaka 90, hata hivyo, Wizara ya Nishati na Madini imetoa ofa ya kuwalipia chuo vijana 150 kila mwaka,” alisema Ghasia, lakini wananchi hao waliendelea kumzomea.“Uongo, uongo, hatutaki, hatutaki, huyoo, huyooo” walisikika wakisema wananchi hao, hali iliyomfanya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kuingilia kati, kujaribu kuwatuliza. “Kelele unazozisikia dada (Ghasia) zinaashiria kuna jambo, nafasi hizo 150 hawazipati, kama zinatolewa basi kwa upendeleo,” alisema Nape huku akishangiliwa na wananchi hao.Baada ya hali kutulia kiasi, Ghasia alijaribu kuendelea kutoa ufafanuzi, lakini kitendo cha kuanza kuzungumza, wananchi hao walianza tena kuzomea. “Kila mtu amelelewa katika mazingira tofauti, hilo halinihusu…watu wangu wa Mtwara vijijini wamenielewa,” alisema Ghasia na kuteremka jukwaani hali iliyozidisha kelele za kumzomea.Nape alisawazisha mambo kwa kusema, hoja ya wananchi hao imechukuliwa na itawasilishwa kwa Serikali ili kuona namna ambavyo inaweza kukaa na wananchi hao na kuweka maslahi yao mbele. Ilivyoanza Panzia la zomea zomea lilifunguliwa na Chiza alipopanda jukwaani kujibu hoja ya kuyumba kwa soko la zao la korosho, ambapo wananchi walimpinga baadhi ya kauli alizozitoa.“Tatizo la korosho ni baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika na wengine ni watendaji wa Serikali …nipo hapa na wala siondoki, nitalishughulikia hili ili korosho zinunuliwe” alisema Chiza huku sauti za wananchi zikimpinga kwa kusema “uongooo”. Hata hivyo, Chiza aliweza kukabiliana na hali ya zomeazomea jukwaani baada ya watuliza wananchi kwa kusisitiza kuwa ataendelea kuwapo Mtwara, kushughulikia tatizo hilo ili ununuzi uendelee.Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwanri alipata wakati mgumu mara alipopanda jukwaani na kuanza kuzungumzia namna ya kumaliza kero ndogondogo zinazoletwa na mamlaka zake, wananchi walikuwa wanazoea “huyoo…hatutaki” lakini baada ya kuanza kuongea alionekana kuiteka hadhira na mambo yakawa shwari. “ “Tumesema wauza vitumbua, wasibughudhiwe … mkurugenzi njoo jukwani, nakuagiza kuanzia leo marufuku wanafunzi kurudishwa shuleni kwa sababu ya michango” alisema Mwanri huku akishangiliwa.Awali Kinana alisema mkutano huo unalenga kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi ambazo zinawezakuwa kikwazo kwa chama hicho kuingia madarakani mwaka 2015. Katibu mkuu huyo wa chama tawala alisema umefika wakati wa chama kusimamia utendaji wa Serikali kutatua kero za wananchi wa mkoa wa Mtwara ikiwa ni pamoja na kuyumba kwa soko la korosho na gesi.“Najua hapa kuna kero kubwa mbili, korosho na gesi, nimekuja na Mawaziri hapa watatoa majibu leo” alisema Kinana huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu ulioudhuria mkutano huo. Chanzo: Mwananchi Newspaper, Nov 2012

Thursday, November 22, 2012

Kinana atangaza vita viwanda vya korosho

“Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi ama virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii, nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ametangaza vita dhidi ya vigogo walionunua viwanda vya kubangua korosho, lakini wakashindwa kuviendeleza na akaitaka Serikali iwanyang’anye.
Amesema vigogo hao ambao walinunua viwanda 12 vya kubangua korosho vya Serikali hivi sasa havifanyi kazi na vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia mazao. Kinana alisema hayo jana mkoani Mtwara wakati akiwahutubia wanachama wa tawi la CCM katika Kijiji cha Mkunwa kilichopo katika Wilaya ya Mtwara. “Wamenunua viwanda vyetu, lakini wameshindwa kuviendeleza, ajira zimepotea, wananchi wa Mtwara wanaendelea kuwa maskini,” alisema Kinana. Alisema wakati viwanda hivyo vikifanya kazi, kila kimoja kiliweza kuajiri watu wengi, lakini sasa hivi vijana wanakosa kazi kwa sababu viwanda hivyo vimefungwa. “Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi ama virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii, nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” alisema Kinana. Alisema maghala ya viwanda hivyo hivi sasa yanahifadhi korosho ambazo hazijabanguliwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Uchina na India. “Korosho zinasafirishwa na vigogo hao kwenda nje ya nchi zikiwa hazijabanguliwa, matokeo yake wakulima wanapata fedha kidogo kwa sababu wao hawabangui korosho bali zinakwenda kubanguliwa nje ya nchi,” alisema Kinana. Alisema vigogo hao ndio waliovuruga uchumi wa mikoa ya Kusini kwa sababu ajira zilizokuwa zikipatikana zamani hivi sasa hazipo kwa sababu wameua viwanda walivyokabidhiwa. Alibainisha kuwa vigogo hao wamekuwa wakitumia viwanda hivyo kuombea mikopo kwenye benki ili kuendeleza biashara ya korosho ambayo inamnyonya mkulima na kuwafaidisha wao. “Tumechoka, sasa ni lazima tukatae unyonyaji huu. Wabunge wa Mtwara ni lazima tusaidiane kulisimamia hili hata kama kwa kutunga sheria itakayovilinda viwanda vyetu,” alisema. Aliongeza: “Kama wao wamenunua viwanda wakakiuka masharti yanayowataka kuviendeleza, sisi tutashindwa vipi kutunga sheria itakayowalinda wakulima na viwanda vyetu?” alihoji Kinana. Akizungumzia zaidi zao hilo, Kinana alisema wanaofaidika nalo siyo wakulima bali wafanyabiashara na wajanja wachache ambao sasa wamesababisha malalamiko kuendelea kila mwaka. Kinana alisema hayo baada ya wananchi wengi kumlalamikia kwamba walikuwa hawajapata malipo ya korosho zilizokopwa na vyama vya ushirika. “Nashukuru Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza ataendelea kubaki hapa Mtwara ili kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya wakulima wa Korosho,” alisema. Awabana viongozi CCM Akizungumzia uhai wa chama hicho, Kinana alisema kuanzia sasa yeye na viongozi wenzake watakuwa wakitembelea matawi na mashina ya chama hicho kwa sababu huko ndiko kwa wenye chama. “Tulijisahau kidogo huko nyuma, tukawa tunafanya mikutano kwenye mikoa, lakini sasa kila kiongozi wa chama anatakiwa kwenda kwenye mashina na matawi ili kufahamu matatizo ya wanachama,” alisema Kinana. Kinana aliahidi kutoa mifuko ya saruji 100 , mabati na mbao kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ili wanakijiji wa Mkunwa waweze kupata huduma za afya. Kwa upande wake, Chiza ambaye yuko katika ziara hiyo, alisema ataendelea kubaki katika mkoa wa Mtwara na Lindi ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wakulima wa korosho an alisema “Nikiwa katika mikoa hii nitakutana na wenye benki ili kuzungumza nao namna tunavyoweza kupata fedha za wakulima wa korosho”. Awali wakulima wa korosho wa kijiji hicho wakizungumza mbele ya viongozi hao walisema licha ya kuuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani bado hawajalipwa fedha zao. “Tumeuza korosho, lakini ni muda mrefu hatujapata awamu ya pili ya fedha zetu, tunaomba chama kitusaidie,” alisema Hadija Hassan ambaye aliungwa mkono na wanakijiji wengine ambao walisema hiyo ndiyo kero yao kubwa. Akijibu hoja hiyo, Kaimu Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Mtwara, Lilanga Mohamed alisema “Tumekuwa tukifuatilia benki na tumeahidiwa kwamba wiki ijayo fedha hizo zitapatikana na wakulima wataanza kulipwa,” alisema Lilanga.

Tuesday, November 20, 2012

Mradi wa kusafirisha Gesi kutoka Mtwara - Dar es Salaam - Tanga - Mombasa

Huu ulikuwa ni Mchango wa Mh. Blandes, Gosbert Begumisa[CCM, Karagwe] kwenye Bunge la Bajeti tar 19 Agosti 2011 "Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa kuleta hotuba nzuri ya Bajeti." Aliongeza "Mheshimiwa Spika, mradi wa kutandaza bomba la gesi asilia kutoka Mtwara - Dar es Salaam - Tanga - Mombasa, katika Bajeti mbalimbali zilizopita za Wizara hii zilitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa nia ya kutandaza bomba la gesi kutoka Mtwara - Dar es Salaam - Tanga hadi Mombasa. Kule Mombasa gesi hii ilikuwa itumike kuzalisha umeme, inawezekana nia hii ilikuwa njema lakini kutokana na hali ya upungufu wa umeme hapa nchini na uhaba wa gesi nashauri tusipele ke gesi nje ya nchi wakati sisi wenyewe tunashida ya umeme. Tusubiri hadi pale tutakapopata umeme na gesi ya ziada ndio tufikirie kupeleka gesi nje ya nchi. Kwa sasa nia ya kupeleka gesi Mombasa isitishwe, ni vizuri katika kufanya majumuisho Mheshimiwa Waziri atupe msimamo wa Serikali katika suala hili". Hii ni taarifa ya Hansard ya Bunge na hakuna aliyewahi kusikika akikanusha mradi huu. Je, wanakusini wategemee kukombolewa na raslimali walizonazo kutoka kwenye lindi la umaskini? Toa maoni yako

Friday, November 09, 2012

Wanakusini mna maoni gani kuhusu maamuzi ya Serikali kusafirisha gesi ya Songosongo (Kilwa, Lindi) na sasa Mnazi Bay (Mtwara) hadi Dar es Salaam na baadae Tanga kwa kufulia umeme, kutumika majumbani na kujengea viwanda vya mbolea?
Tafadhali tunaomba maoni yako ya dhati kwenye hili kwa ustawi wa wananchi maskini wa Lindi na Mtwara.

Thursday, August 30, 2012

Kikao cha SEDO kwa Wanakusini Jpili tar 2nd Sept 2012 Mikocheni, Dar es Salaam

Habari za kazi? Natumai wote mu wazima.

Napenda kuwaarifu kikao cha maendeleo cha wadau wa kusini yaani Lindi na Mtwara kinatarajiwa kufanyika siku ya Jumapili, tarehe 2 Septemba 2012, saa 8 mchana nyumbani kwa Balozi General Makame Rashid pale Mikocheni jirani na flats za TPDC. Agenda za mkutano pamoja na zingine ni kujadili mipango ya maendeleo kusini, mradi wa ufundishaji sekondari za kusini na kutengeneza vitambulisho vya wanachama wa SEDO.

Tunaombwa tuhudhurie kwa wingi na kila mmoja amuarifu mdau wa kusini juu ya mkutano huu. Tafadhali pia, tunaombwa tuendelee kuuboresha mfuko wa taasisi yetu kwa manufaa ya ndugu zetu kusini na sisi pia kama wanachama.

Karibuni nyote tushiriki kwa DHATI kuijenga Lindi na Mtwara.

Geoffrey Idelphonce Mwambe
Chairman
South Eastern Development Organization (SEDO)
P.O.Box 14292 Dar es Salaam
Tel: +255 784 509891; +255 785 271644; +255 782503840
Blog: http://kusiniforum.blogspot.com

Monday, August 13, 2012

Kiwanda Kipya cha Simenti Mtwara Kusisimua Uchumi wa Kusini

"Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (katikati) akionyeshwa mchoro wa ramani na mtaalamu wa udongo, Bw. John Olalokun (kushoto) wa kiwanda cha Simenti cha Dangote kinachotarajiwa kujengwa mkoani Mtwara. Bw. Mbilinyi alifanya ziara hiyo kuangalia maendeleo ya mradi huo mwishoni mwa wiki. Kulia ni meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Dilip Musale.Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akimsikiliza kwa makini mtaalamu wa udongo, Bw. John Olalokun wa kiwanda cha Simenti cha Dangote kinachotarajiwa kujengwa mkoani Mtwara katika ziara aliyoifanya kutembelea eneo hilo na kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Ujenzi huo unafanywa na mwekezaji na tajiri maarufu raia wa Nigeria, Bw. Aliko Dangote".

Na Mwandishi wetu, Mtwara

Zaidi ya tani milioni mbili za saruji zinatarajiwa kuzalishwa nchini kwa mwaka mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kutengenezea simenti cha Dangote katika Mkoa wa Mtwara.

Pamoja na kiwango hicho cha simenti kuzalishwa, pia inatarajiwa kupatikana kwa ajira 400 za kudumu ujenzi huo utakapokamilika.

Uwekezaji huu unafanywa na tajiri maarufu raia wa Nigeria, Bw. Aliko Dangote ambaye ana vitega uchumi vikubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi alipofanya ziara katika eneo ambapo uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote unatarajia kuanza Mkoani Mtwara.

“Kukamilika kwa mradi huu mkubwa katika mkoa wa Mtwara kutazalisha zaidi ya tani milioni mbili za saruji, lakini pia ajira za kudumu zaidi ya mia nne zitapatikana, hii itasaidia kukuza uchumi wa watu wa kusini na kuongeza pato la taifa kwa ujumla,” alisema Mbilinyi mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mkoani humo.

Akielezea umuhimu wa ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kinatarajia kukamilika baada ya miezi kumi na nane, Bw. Mbilinyi alisema uwekezaji wa aina hii si tu utaweza kuzalisha ajira nyingi kwa watanzania bali utaongeza kasi ya kuchochea uwekezaji zaidi katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.

“Kwa takwimu tulizonazo, hadi kufikia mwaka 2011 tulikua na upungufu wa zaidi ya tani milioni moja za simenti, hivyo kiwanda hiki kitasaidia kuondoa upungufu huu,” alisema.

Alisisitiza kuwa mazingira mazuri yalijengwa na serikali pamoja na sekta binafsi ndio yaliyosaidia kumpata muwekezaji huyu mkubwa wa simenti katika Bara la Afrika kuja kuwekeza hapa Tanzania.

“Juhudi zetu zote kwa upande wa serikali na kwa upande wa sekta binafsi ndizo zilizosababisha muwekezaji huyu mkubwa kuja hapa kwetu hasa katika mkoa wa mtwara na kanda ya kusini kwa ujumla,” alisema na kuongeza kwamba serikali itaendelea kujenga mazingira bora ya kuvutia wawekezaji, si tu kwa viwanda vya simenti bali hata kwa viwanda vya aina nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, alisema ujenzi wa kisasa siku zote unahitaji saruji hivyo uwekezaji huo umekua mkombozi kwa watu wa mikoa ya kusini na Tanzania kwa ujumla.

“Kukamilika kwa kiwanda hiki kutakuwa na faida kubwa sana kwa mkoa huu, hasa kiuchumi kutokana na mtwara kuwa na mafuta pamoja na gesi asilia ambayo inaweza kuongeza asilimia kubwa ya pato la Taifa na kuondoa umasikini katika nchi,” alisema Simbakalia.

Bwana Simbakalia aliongeza kuwa ni ukweli usiopingika kuwa Mkoa wake una ufursa nyingi sana za uwekezaji na miongoni mwao bado hazijafanyiwa uwekezaji unaotakiwa.

Naye mtaalamu wa masuala ya utafiti wa udongo kutoka katika kampuni ya simenti ya Dangote Bw. John Olalokun, amesema, wamefanya utafiti wa kutosha na kuona kuwa malighafi nyingi zinapatikana katika eneo husika na kuongeza kuwa hiyo ni faida kwao katika kuzalisha simenti kwa wingi mkoani humo.

Aliongeza kuwa kati ya walivyoangalia kufanya uwekezaji katika mkoa wa Mtwara ni kutokana na upungufu uliopo wa simenti katika mikoa ya kusini na hii imetokana na simenti nyingi kuelekezwa katika mikoa ya kaskazini mwa nchi.

Friday, August 03, 2012

Serikali kukabili changamoto ugunduzi wa Gesi

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali inajipanga kukabiliana na changamoto zinazoambatana na ugunduzi wa gesi asilia nchini na kuitaja moja ya changamoto hiyo kuwa ni ufisadi unaoweza kusababisha Watanzania wasinufaike na rasilimali hiyo.


Rais Kikwete alisema hayo jana Ikulu alipokutana na wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakiwamo wakurugenzi, wahariri wakuu, wahariri watendaji na waandishi wa habari waandamizi, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kulihutubia taifa kila mwisho wa mwezi.

Alisema hadi sasa, Tanzania imeshagundua kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 na trilioni 28.9 ambazo zikitumika vizuri, zinaweza kubadili uchumi na maisha ya Watanzania.

Kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta nchini hivi sasa ni 18 zikiwamo zenye uzoefu mkubwa wa kufanya kazi hiyo duniani na kati ya mwaka 1954 na mwaka huu, kati ya visima 61 vilivyochimbwa, 22 vimebainika kuwa na gesi na kati ya hivyo 14 viko nchi kavu na vinane baharini.

“Changamoto nyingine ni jinsi ya kutumia mapato yatokanayo na gesi, maana tusipojipanga tunaweza kukuta kwamba mapato yetu yanaishia mikononi mwa watu wachache halafu mwishoni mwa siku wao wakaneemeka, taifa likakonda na wananchi pia wakakonda,” alisema kuongeza:

“Hivyo sisi tunasema lazima tujipange, tunaweza kuunda chombo kama gas revenue fund (mfuko wa mapato ya gesi) na tukaamua kwamba fedha zetu zitunzwe humo ili kila tunapozitumia tufahamu zimefanyia nini na zinalisaidia taifa kwa kufanya kitu gani.”

Alisema hatua hizo zisipochukuliwa, gesi inaweza kwisha halafu taifa likajikuta hakuna kitu chochote muhimu lilichofanya kutokana na mapato ya rasilimali hiyo.

Rais Kikwete alisema maandalizi mengine yanayofanywa na Serikali ni kuandaa sera ya gesi asilia, kutunga sheria ya kusimamia sekta hiyo na kurekebisha sheria iliyopo ya utafutaji wa gesi na petroli.

Alisema changamoto nyingine ambayo Serikali inajipanga kukabiliana nayo ni kuandaa wataalamu wa kusimamia sekta ya gesi katika maeneo mbalimbali, wakiwamo wa hesabu zinazohusiana na sekta hiyo, wahandisi, mafundi, wanasheria na wataalamu wa mikataba ya gesi.

Rais alisema maandalizi hayo ni muhimu na kwamba yasipofanyika, taifa linaweza kujikuta likidhulumiwa au kupunjwa mapato yanayotokana na rasilimali hiyo, au kulalamika kwamba limepunjwa hata kama halijatendewa hivyo.

Kutokana na hali hiyo, alisema wataalamu wanaandaliwa hivi sasa na taasisi kadhaa za elimu ya juu nchini zimeanzisha masomo na kozi mbalimbali zinazohusu masuala ya usimamizi wa petroli na kwamba kozi hizo zitaanza kutolewa katika mwaka ujao wa masomo.

Aliyataja maandalizi mengine kuwa ni kuanzisha kozi za ufundi mchundo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Mtwara, ambako Wizara ya Nishati na Madini tayari imetangaza mpango wa kuwafadhili wanafunzi 50 chuoni hapo ambao watatoka mkoani Mtwara.

“Pia wizara hii ina mpango wa kusomesha wataalamu kati ya 40 na 50 kuanzia sasa na mwaka 2016 katika fani mbalimbali za masuala haya ya gesi na lengo ni kwamba tuwe tayari katika maeneo yote muhimu ya kuwa wasimamizi na kuepuka kazi zote kuchukuliwa na Wafilipino (wageni),” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema msingi wa kuwapata wataalamu lazima uwe endelevu, kwa kuhimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati katika elimu ya msingi na sekondari.

Mgomo wa walimu
Kuhusu mgomo wa walimu, Rais Kikwete alisema Serikali inawathamini watumishi hao wa umma na kwamba kamwe haiwezi kuwadharau, isipokuwa madai yao ya sasa ni makubwa mno na “hayatekelezeki”.

“Ikiwa tutaamua kulipa kama wanavyotaka ina maana kwamba Serikali itumie kiasi cha Sh6.5 trilioni kwa ajili ya mishahara tu. Makusanyo yetu ya ndani ni Sh8 trilioni, hapo ina maana kwamba tutakuwa tunafanya kazi ya kuwalipa watumishi wa umma tu,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Sasa tukifikia hapo hata wananchi watagoma, watasema hawa watumishi 500,000 wa Serikali wamejikusanyia hela yote ili wajinufaishe wao peke yao, kwa sababu hatutaweza kununua dawa wala kutoa huduma nyingine yoyote, itakuwa ni mishahara tu.”

Alisema Serikali inasubiri uamuzi wa Mahakama unaotarajiwa kutolewa leo na kwamba jambo linalomsikitisha ni taarifa kwamba baadhi ya walimu wamekuwa wakiwapiga na kuwatishia wenzao ambao hawakugoma.

“Mimi ninasema, kama wewe umegoma, basi siyo vizuri kwenda kum-harass (kumbugudhi) ambaye hakugoma, wale ambao wana uchungu na watoto waacheni jamani waingie darasani, wafundishe,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali iko tayari kuendelea na mazungumzo na walimu na kwamba anaamini kuwa kuna wakati watafikia mwafaka na kurejesha hali ya ufundishaji kama ilivyokuwa mwanzo.

Vita dhidi ya rushwa
Kadhalika, Rais Kikwete alizungumzia vita ya rushwa na kusema bado ni tatizo kubwa nchini, licha ya jitihada ambazo Serikali imefanya za kuimarisha taasisi za kupambana na tatizo hilo.

“Hii si kazi ya Serikali pekee, inahusisha taasisi zote na dhamana hii tumewapa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na huwa hatuwaingilii katika kazi yao, lakini tunasaidiana hapa na pale kuona walau tunapiga hatua,” alisema.

Kuhusu kashfa ya rada, Rais Kikwete alisema Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo kutokana ukweli kwamba hata, Uingereza walikana Kampuni ya BAE Systems kutoa rushwa na badala yake wakasema ilikosea katika kuandika hesabu zake.

“Sasa hapo sisi tunaanzia wapi, maana kwenye asili ya tukio hili, wanasema hakuna rushwa, kwa hiyo wanasheria wetu tukiwauliza nao wanahoji kwamba tunaanzia wapi katika suala hili,” alisema.
Kuhusu kashfa ya Kagoda ambayo ni sehemu ya ufisadi wa wizi kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa), kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Rais Kikwete alisema taarifa alizonazo ni kwamba suala hilo bado linachunguzwa.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

Tuesday, July 31, 2012

Vurugu Zaibuka Upya Malipo ya Korosho Tandahimba

Taarifa kutoka Wilaya ya Tandahimba zinasema kuwa vurugu zimeibuka upya wilayani humo kufuatia kutokamilishiwa malipo kwa wakulima wa korosho kufuatia kulipwa kwa awamu ya pili ya malipo hayo baada ya vurugu za awali.

SEDO inaiomba serikali kuwathamini wananchi wa kusini kwa kuhakikisha wanapata stahili ya jasho lao ili liwasaidie kupata mahitaji ya lazima kimaisha lakini pia kuwapeeleka watoto shule ili kuikwamua kusini kutoka kwenye umaskini. Mfumo huu wa stakabadhi ghalani unaonekana kulalamikiwa sana na wakulima wa korosho hasa wa mikoa ya kusini kuliko mahali kwingineko nchini.

Tunahitaji wanakusini kuungana na kuona kadhia hii inayotufanya kila uchao tunarudi nyuma kimaendeleo inaondoka kusini.