Wadau wa kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara kupitia taasisi yao ya maendeleo ya kusini mashariki (SEDO) walikutana siku ya tarehe 15 Aprili 2012 mtoni kijichi, DSM nyumbani kwa mmoja wa wanakusini. Katika kikao hicho, wanakusini walirudia wito kwa kila mmoja kujitoa kwa hali na mali na kwa nafasi yake kuhakikisha maslahi ya wananchi wa kusini yanalindwa na kuzingatiwa.
Mambo mengi yalijadiliwa ikiwa ni pamoja na:
1. Kuimarisha nia ya ushirikiano kati ya wanakusini ili kuondoa udhaifu uliojengeka miaka nenda rudi ya utengano, kutopendana, kujijali binafsi na kutukuza marafiki wa nje ya Lindi na Mtwara kwa kupuuza undugu wetu;
2. kuhamasisha michango ya Fund raising iliyofanyika kwa mafanikio makubwa tarehe 18 Novemba 2011 pale Karimjee Hall, DSM ili fedha zikusanywe mapema na hivyo kufanikisha malengo yake;
3. Kutathmini kwa kina mikakati ya kuboresha sekta ya elimu kusini;
4. Kufuatilia uuzaji wa zao la korosho ambapo wananchi walio wengi na wanaotegemea korosho kama chanzo cha kipato chao cha mwaka hawajalipwa pesa zao na hivyo kuwafanya washindwe kumudu kujipatia mahitaji yao ya kila siku, kupeleka watoto shule na kujitibu pale wanapougua. Uongozi wa SEDO ulitoa taarifa ya ufuatiliaji huo ambapo uliarifiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya korosho kuwa makubaliano yameshafikiwa na vyama vya ushirika kuweza kupata dhamana ya serikali ili walipie tani karibu 85,000 zilizomo maghalani. Tayari tani zaidi 77,000 zilishanunuliwa na vyama hivyo vya ushirika.
5. Taarifa ya uongozi wa SEDO juu ya umaliziaji wa kilomita 60 za barabara ya kusini eneo la Ndundu - Somanga ambapo taarifa ni kuwa mkandarasi amelipwa pesa hivi karibuni na anafanya juhudi za kumalizia eneo lililobakia ambalo ni kama kilomita 40 hivi.
6. Wanakusini wameazimia kuwakumbusha wanachama wa SEDO na wanakusini wengine waweze kujumuika kwa pamoja, tuache utengano na kujiimarisha katika umoja ili kupitia SEDO mipango ya maendeleo ya kusini iwe na manufaa kwa ndugu zetu kule.
Kikao kijacho ni tarehe 06 Mei 2012, mahali pa kikao mtaarifiwa.
Imetolewa na:
SEDO Sekretariati
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment