MAELFU ya wakulima wa korosho wa Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara jana wameandamana kuishinikiza Serikali iwalipe malipo ya pili ya mauzo ya zao hilo, kama ilivyoelekezwa na Rais Jakaya Kikwete. Maandamano hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Wananchi (CUF) wilayani humo, yalianzia ofisi za chama hicho saa 5:38 asubuhi na kuishia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo saa 6:10 mchana kabla ya kwenda kwenye mkutano. Maduka yalifungwa na shughuli zingine zilisimama kwa muda kuanzia asubuhi hadi baada ya maandamano na kusababisha watu kukosa huduma. Wakulima hao walibeba mabango yaliyo na ujumbe mbalimbali ambapo baadhi yalisomeka; “ahadi za kizushi tumechoka, ‘tulipe tusepe’… ‘fedha kwanza mazungumzo baadae ‘….’muda wa kusubiri umepita na agizo la Rais litekelezwe,” lilieleza bango hilo.
Kinyume na matarajio ya wengi, maandamano hayo ambayo yalitarajiwa kupokewa na Mkuu wa Wilaya, Hasna Mwilima yalikosa mpokeaji na hivyo kuwalazimu wakulima hao kukaa kwa karibu saa moja juani wakimsubiri Mkuu huyo wa Wilaya ili ayapokee.
Faragha zilitawala kwa viongozi wa CUF walioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Julius Mtatiro na hatimaye Mwilima alipokea maandamano hayo saa 6:59 mchana.
Akisoma risala ya wakulima hao, Katibu wa CUF wa Wilaya ya Tandahimba, Abasi Namanema alisema tangu kutolewa kwa tamko la Rais la kutaka wakulima hao walipwe malipo ya pili ya Sh 350 kwa kilo za korosho walizouza hakuna utekelezaji wa agizo hilo .
Mwilima alisema; “tatizo la korosho si la Tandahimba pekee, ni la mkoa mzima … kama mlikuja mkidhani kuwa DC atatangaza leo kuwa malipo ya pili yatalipwa lini mtakuwa mnanionea.”
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Michezo Tandahimba, Mtatiro alisema hawakuridhishwa na majibu ya Mwilima na kutafsiri kuwa kitendo hicho ni sawa na kutojua majukumu yake na hivyo hawana imani kama anaweza kuwa msaada katika hilo.
Chanzo: Gazeti la HabariLeo
No comments:
Post a Comment