Thursday, April 12, 2012

Masikitiko kwa Wanakusini ... Viwanda nchini vimekufa, Korosho yabanguliwa nje

HIVI karibuni wachumi kutoka China na Vietnam wamesema umasikini unaoikabili Tanzania pamoja na mambo mengine unatokana, viongozi kuwa na maneno mengi kuliko vitendo.

Walisema hayo mbele ya Rais Jakaya Kikwete na kukosoa mchakato wa ubinafsishaji, uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ambao umebinafsisha na viwanda vingi vya msingi ambavyo sasa vimekufa.

Wakichangia mada katika mkutano wa 17 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini Tanzania (Repoa), wachumi hao wanasema Tanzania haikuwa nchi ya kutegemea misaada kutoka kwa wahisani, bali ilipaswa kujitegemea.

Ashangaa serikali kubinafsiha viwanda
Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya Vietnam anasema inasikitisha kuona Tanzania ina kila rasilimali, lakini ni nchi masikini ya kutupwa.

Nchi imebinafsisha viwanda bila umakini na matokeo yake viwanda vingi vimekufa. Kwetu suala la ubinafsishaji tulikuwa makini na Serikali inamiliki viwanda vingi ambavyo vinatoa ajira.

Vietnam hatulimi korosho, lakini tuna viwanda vingi vya kubangua korosho, tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania, anasema Profesa DucDinh.

Profesa DocDinh anaishangaa Tanzania ambayo inalima korosho, lakini bila viongozi wake kufanya uchambuzi wa kina, walibinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo na kusababisha hali mbaya kwa zao hilo hivi sasa.

Utabinafsisha vipi viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo na ambacho kinategemewa kwa ailimia 80 na wananchi wake? anahoji.

Anasema kama Tanzania ina nia ya dhati ya kupunguza umasikini kwa wananchi wake, inatakiwa kujipanga na kusaidia kuikuza sekta ya kilimo.

Sekta ya kilimo iboreshwe kwa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kujenga miundombinu na wakulima kutumia mbegu bora na mbolea, anasema.

Kauli hiyo ya Profesa DocDinh imekuja ikiwa ni siku chache tu baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kuishauri serikali kutaifisha viwanda vyote vya korosho nchini kutoka mikononi mwa watu binafsi.

POAC inatoa ushauri huo baada ya kubaini kwamba watu waliopewa viwanda hivyo wameshindwa kazi na kukiuka mkataba wa mauzo ulikouwapo awali.

POAC imetoa ushauri huo baada ya kutembelea wakulima wa korosho mkoani Mtwara na Lindi na kupokea taarifa kutoka Bodi ya Korosho ambayo imeonyesha kuwa viwanda 12 ambavyo serikali ilikuwa inavimiliki na kuvibinafsisha hivi sasa vimegeuzwa kuwa maghala.


Viwanda vilivyobinafsishwa vinamilikiwa na raia wenye asili ya kiasia ambao wamevigeuza maghala na kusafirisha korosho nchini India kwa ajili ya kubangua badala ya kutumia viwanda hivyo kubangua.

Viwanda vitaifishwe

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe anasema ni lazima serikali itaifishwe viwanda hivyo kwa kuwa hali ya wakulima wa korosho nchini iko taabani baada ya viwanda vya kubangua zao hilo kubinafsishwa

Zitto ameshangazwa na hali ya wakulima wa Korosho jinsi ilivyo mbaya kutokana na viwanda hivyo kutofanya kazi na pia ameshauri wanaomiliki wanyang'anywe kwa kuwa wamekiuka mikataba ya makubaliano ya mauzo.

Kwa kuwa viwanda vyote vimeshindwa kazi wanaomiliki sasa hivi wanyanganywe kwa sababu hali za wakulima wa korosho ni mbaya na hazionyeshi matumaini,anasema Zitto.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma(CHC), mbele ya POAC imeonyesha baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa vimebadilishwa kuwa maghala ya kuhifadhia bidhaa.

Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa CHC, Dome Malosha kwa Mwenyekiti wa POAC, imeonyesha kuwa kati ya viwanda 12 vilivyobinafsishwa ni viwanda viwili tu vinafanya kazi.

Katika taarifa ya Malosha anasema viwanda ambavyo havifanyi kazi ni Mtwara, Newala I, Masasi, Nachingwea, Mtama, Likombe, Lindi, Kibaha na Tanita I na Tanita II.

Viwanda vinavyofanya kazi ni Newala II na Tunduru, lakini vyote vinafanya kazi chini ya uwezo halisi wa kiwanda,imeeleza taarifa ya Malosha.

Anasema viwanda hivyo viwili awali vilikuwa vina uwezo wa kubangua korosho tani 10,000 kwa mwaka kila kimoja, lakini hivi sasa vinabangua tani 2,000 tu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Ayubu Mbawa akizungumza mbele ya kamati ya POAC anasema hali imekuwa mbaya kotokana na viwanda hivyo kutokufanya kazi hivyo maamuzi magumu yanahitajika.

Anasema viwanda vilivyobinafsishwa vilikufa baada ya miaka miwili tangu kubinafsishwa.

Taarifa ya Mbawa inaeleza kwamba viwanda hivyo havifanyi kazi kwa sababu wamiliki hawana fedha za kutosha za uendeshaji na kuwapo kwa tatizo la umeme na ukosefu wa maji.

Lakini Mbawa hakubaliani na hoja hizo kwa kuwa umeme upo wa kutosha na mashine zipo katika hali nzuri katika baadhi ya viwanda

Anasema wakulima wamezalisha tani 155,000 za korosho ambazo hazijawahi kazalishwa tangu nchi ipate uhuru, lakini zinashindwa kubanguliwa kwa sababu viwanda vilivyopo vina uwezo wa kubangua tani 4,000 tu kwa mwaka mzima.

Mbawa anasema hali hiyo imesababisha wakulima kuuza korosho ambazo hazijabanguliwa nje ya nchi na kutoa ajira katika viwanda vya ubanguaji vilivyoko nje na jambo ambalo kama viwanda vyetu vingekuwa vinafanya kazi, ajira hizo zingebaki nchini.

Tani 85,000 zakwama ghalani
Pia hali hiyo imesababisha nusu ya mavuno ya mwaka huu kushindwa kupata masoko nje ya nchi kutokana na korosho kutobanguliwa.

Hivi sasa tuna tani 85,000 zimekwama kwenye maghala kwa kukosa wanunuzi wa nje na hakuna matumaini ya kupatikana kwa soko tangu kusimama kwa kuuza zao hilo nje ya nchi,anasema Mbawa.

Anasema hali hiyo imesababisha wakulima wakose fedha baada ya kuuza mazao yao kwenye vyama vya ushirika kwa kutumia mpango wa stakabaadhi ghalani.

Mbawa anasema mpango wa kubinafsisha viwanda, umeshindwa kufikia matarajio yaliyokuwa yakitegemewa tangu awali na kusababisha umasikini kwa wakulima wa Korosho nchini.

Tulitegemea kuwa ubinafsishwaji wa viwanda ungesaidia uzalishaji na kuongeza ufanisi katika ubanguaji wa Korosho, lakini imekuwa kinyume,anasema.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Mangungu Murtaza ambaye ni mjumbe wa POAC, aliitaka bodi ya korosho itafute masoko nje ya nchi kwa kutumia balozi za Tanzania zilizoko huko.

Acheni kukaa tu, ziandikeni balozi zetu nje ya nchi na mfuatilie ili mpate masoko ya korosho katika nchi mbalimbali,anasema Mangungu.

Kwa upande wa chama cha wakulima wa korosho kinasema mwaka huu biashara hiyo siyo mzuri kwa kuwa wameshindwa kupata fedha ya ununuzi wa zao hilo kukwama.

Mhasibu Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Masasi na Mtwara, Clement Alex anasema wanunuzi wa zao hilo wamekuwa wakijipangia bei wenyewe kwa kupitia tenda kwenye mnada.

Anasema bei ya zao hilo awali ilikuwa Sh2,000 mpaka Sh2,500 kwa kilo Oktoba mwaka jana, lakini iliaanza kushuka na kufikia Sh1,500 kwa kilo jambo ambalo limesabisha wakulima washindwe kuuza kwa kuwa itakuwa ni hasara.

Tulikuwa tuna tani 44,000 na tumeuza tani 16,000 na bei imeshuka, hatuwezi kuuza tena, zimebaki tani 28,000 ambazo ziko ghalani mpaka bei itakapopanda tena,anasema Alex.

Anasema hali ya wakulima ni mbaya kutokana na kukwama kwa biashara hiyo na kufafanua kwamba chama kinanunua korosho kutoka kwa wakulima kwa Sh1,200 na kuisafirisha mashambani mpaka kiwandani na kusababisha gharama kuwa juu zaidi.

Baada ya kununua kwa wakulima na kuiuza tunawalipa wakulima kwa awamu mbili, awamu ya kwanza Sh850 ambayo ni sawa na asilimia 70 na Sh350 ambayo ni awamu ya pili sawa na asilimia 30 ukijumlisha unapata 1,200,anasema Alex.

Anasema viwanda hivyo kushindwa kufanya kazi vimesababisha kukosekana kwa ajira.Halmashauri yakosa mapato.

Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara imeshindwa kukusanya mapato ya ndani kwa asilimia 87.79 katika mwaka wa fedha 2011/12 baada ya kuyumba kwa soko la zao hilo.

Mweka Hazina wa wilaya hiyo, Charles Genge anasema hali hiyo imesababisha kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo ya halmashauri hiyo na kuathiri huduma za jamii.

Chanzo:
Habari na Boniface Meena,
Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment