Wednesday, October 05, 2011

Mkuchika atangaza vita dhidi ya watumishi hewa

SERIKALI imesema itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wakuu wa idara katika halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji ambazo zitakutwa na watumishi hewa wanaolipwa mishahara. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George Mkuchika alisema hayo wakati akizungumza na wakuu wa idara na madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Mwanga. Katika ziara hiyo maalumu kwa halmashauri ya Mwanga na Rombo zilizopata hati chafu, Mkuchika alisema serikali imekuwa ikilipa mishahara kwa watumishi waliokufa, kustaafu au kufukuzwa kazi jambo ambalo kwa namna moja au nyingine inawezeshwa na wakuu wa idara husika. Waziri Mkuchika alisema ulipwaji wa mishahara hewa umekuwa ukiigharimu serikali mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kuendesha miradi ya maendeleo kwa wananchi wa mijini na vijijini. Alisema wakuu wa idara husika watawajibishwa kutokana na ukweli kwamba watumishi hewa wanaolipwa mishahara hiyo wanafahamika na inawezekana ni mtandao wa kundi la watumishi ambao wanafaidika na mishahara hiyo. “Yupo mmoja wa watumishi halmashauri ya wilaya ya Newala ambaye alifariki lakini mtumishi mwenzake alileta barua ya kuomba mabadiliko ya akaunti ya marehemu huyo kwamba fedha zake za mshahara awe analipwa yeye na alifanikiwa,” alisema. Alisema mtumishi huyo alifanikiwa kutokana na mkuu wa idara hiyo kutotoa taarifa ya kifo Hazina ili mishahara hiyo isitishwe ingawa baadaye mbinu hizo zilibainika na mtumishi huyo alirejesha fedha hizo na kusimamishwa kazi.

Chanzo - Habari Leo

No comments:

Post a Comment