Wednesday, October 05, 2011

Mradi wa kuzalisha umeme wa Mg 120 waiva

Mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo Kijiji cha Ruanda Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, utaanza kuzalisha umeme wa megawati 120 miaka miwili kuanzia sasa baada ya Kampuni ya TANCOAL Energy inayomiliki mgodi huo kupata leseni ya biashara hiyo. Shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe zilizinduliwa rasmi hivi karibuni na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk.Chrisant Mzindakaya. Mgodi huo, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa asilimia 70. Waziri Chami alisema mradi huo utaleta ukombozi mkubwa kwa Tanzania ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa nishati ya umeme wa kutosha. “Ukikosa umeme maana yake viwanda haviwezi kufanya kazi, ajira zinapungua, wafanyabiashara wanaathirika na shughuli zingine za uzalishaji mali zinakwama,” alisema na kuongeza kuwa wizara yake itaunga mkono juhudi za kufanikisha mradi huo kwa kuwa inaamini utakua mkombozi wa Taifa katika kipindi kifupi kijacho. Mkurugenzi wa TANCOAL Energy, Graeme Robertson, alisema kwa sasa mradi huo unazalisha tani 30,000 za makaa ya mawe kwa mwezi sawa na tani 360,000 kwa mwaka ambazo huzisambaza katika viwanda vya nchini vikiwemo vya saruji vya Mbeya na Tanga.
Robertson alisema kwa kuanzia TANCOAL Energy itazalisha megawati 120 za umeme katika kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa, lakini uzalishaji huo utakuwa ukiongezeka hadi kufikia megawati 2,000 kwa kuwa eneo hilo la Ngaka lina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe inayozidi tani milioni 250 na kwamba utafiti unaoendelea unaonyesha eneo hilo linaweza kuwa na hifadhi kubwa zaidi. Aliongeza kuwa kampuni hiyo licha ya kuinufaisha Tanzania kwa nishati ya kutosha ya umeme, pia itahakikisha inaisaidia jamii kwa kutoa ajira na kununua bidhaa za kilimo zinazozalishwa na wananchi Naye Dk. Mzindakaya aliwaondoa shaka Watanzania, akisema mradi huo una manufaa makubwa zaidi kwa Tanzania kuliko kwa mwekezaji. Alisema Tanzania pamoja na kunufaika na umiliki wa kampuni ya TANCOAL Energy kwa asilimia 30, pia itanufaika na matokeo ya kuwepo kwa umeme wa kutosha ambao utaihakikishia ustawi wa viwanda, biashara na kilimo. Mzindakaya pia alisema haina sababu kwa taifa kulaumiana kwa kuchelewa kuitumia rasirimali hiyo na badala yake viongozi wachukue hatua ya kuleta maendeleo kwa wananchi. “Hata huu mradi sio watu wote watauunga mkono, wapo watakaoupinga, lakini sisi NDC tutasonga mbele,” alisema Dk. Mzindakaya na kuongeza kuwa NDC na bodi yake hawawezi kuingia mkataba wa kijinga. Katika hatua nyingine Waziri Chami amekanusha vikali uvumi ulioenezwa kuwa Mradi wa Makaa ya mawe wa Ngaka unapanga kujenga mitambo ya kuzalisha umeme katika wilaya ya Kyela mkoani Mbeya badala ya Mbinga Mkoani Ruvuma. Chami alisema uvumi huo hauna ukweli wowote na kwamba, mitambo hiyo itajengwa katika makutano ya Mto Ruhuhu na Mto Ngaka yaliyopo jirani na yanapochimbwa makaa hayo wilayani Mbinga.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment