Friday, September 30, 2011

Serikali yapata mwarobani tatizo la umeme

SERIKALI imedhamiria kumaliza tatizo la umeme nchini na tayari imepata  mkopo wa Dola 1 bilioni za Marekani kwa ajili ya kujenga bomba kubwa la kusafirishia gesi asili kutoka Mnazi Bay mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam. Gesi hiyo itatumika kuzalisha megawati 3,900 za umeme.  Bomba hilo litasaidia kusafisha na kusafirisha gesi kwa ajili ya mitambo ya gesi ya kufua umeme inayomilikiwa kwa ushirikiano wa serikali, taasisi za umma na sekta binafsi, lengo likiwa ni kuliwezesha taifa kuondokana na utegemezi katika umeme unaotokana na maji.  Imesema mradi huo ukikamilika, pia utashusha gharama za umeme kwa asilimia 30. Hivi sasa uniti moja ya umeme inauzwa kwa bei ya  Sh160 na mahitaji ya juu ya nishati hiyo nchi nzima hayazidi megawati 1,000. 
Kwa mujibu wa mkataba, utekelezaji wa  mradi huo unapaswa kuanza wiki ya pili ya mwezi ujao na kukamilika kabla ya Machi mwaka 2013. Hata hivyo  kutokana na ukubwa wa tatizo la umeme, serikali imeomba na kukubaliwa kuwa ukamilike Desemba mwakani.  Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema mkataba huo ni wa kujenga na kupanua bomba la gesi kutoka Mnazi Bay kupitia Songosongo Kisiwani (Kilwa) hadi Dar es Salaam.   Alisema uamuzi wa kutolewa kwa mkopo huo kupitia Benki za China, umetokana na Serikali za Tanzania na China kutiliana saini mikataba ya uhandisi, manunuzi na ujenzi, uliofanyika Septemba 26 mwaka huu.  Alisema mkataba wa mkopo huo wa masharti nafuu na ambao serikali itachangia asilimia 10,utalipwa kwa kipindi cha miaka 20 kwa riba ya asilimia mbili. Waziri Ngeleja alisema” mkataba huo  una vipengele viwili, cha kwanza ni ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mnazi Bay na Songosongo hadi Dar es Salaam lenye urefu wa kilomita 532 na cha pili ni  ujenzi wa mitambo miwili ya kusafisha gesi huko SongoSongo kisiwani na Mnazi Bay,” alisema Ngeleja.  Alisema Shirika la Petroli Tanzania (TPDC)  na CPTDC ambayo ni  kampuni tanzu ya Shirika la Petroli la China (CNPC), zimekubaliana katika vipengele vyote viwili. Kwa mujibu wa Ngeleja, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alifanya ziara China ambako Benki ya Exim ya nchi hiyo, ilikubali kutoa mkopo huo”.
 Alifafanua kuwa mpaka sasa TPDC imeshakabidhiwa Sh6.5 bilioni na serikali kwa ajili ya kulipa fidia wananchi watakaoathirika na mradi huo na kufanya utafiti wa maeneo ya kupitisha mabomba hayo. Utekelezaji wa mradi  Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utakuwa katika awamu mbili. Utaanza na ujenzi wa bomba la gesi utakaohusisha bomba la inchi 24, lenye urefu wa kilomita 25 kutoka Songo Songo Kisiwani hadi Somanga Fungu.  “Pia utaambatana na ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi 36 lenye urefu wa kilomita 207 kutoka Somanga Fungu hadi Dar es Salaam,” 
Alisema kuwa awamu ya pili itahusisha ujenzi wa bomba lenye kipenyo cha inchi 36 lenye urefu wa kilomita 285, kutoka Mnazi Bay hadi Somanga Fungu.  Alisema  bomba la sasa la kusafirisha gesi ni la inchi 16 na kwamba lilianza kutumia mwaka 2004. Alisema kitendo cha kuwa na bomba la inchi 36 kitawezesha upatikanaji wa gesi kiasi cha futi za ujazo 784 milioni kwa siku ikilinganishwa na futi za ujazo 105 milioni zinazozalishwa sasa.  “Hizi zitatumika kwa uzalishaji wa umeme  ambao utafikia megawati 3,900, hivi sasa mahitaji mapya ya umeme utokanao na gesi asili pekee ifikapo 2015 yanakadiriwa kuwa megawati 1583,” alisema Ngeleja.  Alisema bomba linalotumika sasa ambalo linamilikiwa na Songas limezidiwa na kwamba serikali imelazimika kuongeza bomba jingine kutokana na mahitaji ya gesi asili kwa ajili ya uzalishaji umeme.  Alisema kuwa miundombinu ya mradi huo itakuwa chini ya TPDC  kwa asilimia miamoja.  “Faida ya mradi huu ni upatikanaji wa umeme kwa gharama nafuu kwa kuwa ni gharama kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya dizeli, pia gesi hii itakayoletwa Dar es Salaam itafikishwa Bagamoyo kwa ajili ya kuhudumia viwanda chini ya mpango wa EPZ,” alisema Ngeleja. 

Chanzo - Mwananchi

1 comment:

  1. Je, mitambo hiyo ya kufua umeme haiwezi kujengwa Lindi au Mtwara na kuingizwa gridi ya Taifa? Au kusini itafaidika ikiwa itaunganishwa na gridi? Kazi si ndio zinahamishiwa Dar na Tanga na kuwaacha vijana wetu wapigwe na jua na umachinga? Umuhimu wetu Lindi na Mtwara uwe ni kutoa gesi tu? Mirahaba iendelee kulipwa Dar na Tanga? Kuna mdau kaguswa comment namba 25 gazeti la Mwananchi. Je, sisi wenyewe wa kusini tunasemaje? Au ndio "kusini ni kusini tu"?Tukiwa ndio wanakusini tunahitaji kufanya kitu.

    ReplyDelete