Saturday, October 01, 2011

RC Lindi aomba ushirikiano

MKUU mpya wa Mkoa wa Lindi, Alli Nassoro Rufunga amewaomba wananchi, watumishi wa umma, watendaji wa serikali na wakazi wa mkoa, kumpa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha vyema majukumu yake na kuharakisha maendeleo ya mkoa kwa ujumla.  Rufunga ambaye ameteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo, aliyasema hayo kwa nyakati 
tofauti alipokuwa akisalimiana na wananchi katika ziara yake ya kujitambulisha wilaya zote za mkoa huo mwishoni mwa wiki iliyopita.  Mkuu huyo wa Mkoa alisema amefurahishwa na kazi nzuri ya maendeleo, ikiwemo kuboreshwa kwa miundombinu ya mawasiliano ya barabara kuu ya Kibiti-Lindi kwa kiwango cha lami, kuwapo kwa mapinduzi makubwa ya kielimu na huduma nyingine za jamii ambazo  zilisimamamiwa vyema na mtangulizi wake na kwamba anahitaji ushirikiano ili aweze kuendeleza hayo. 
“Nimekuja kwa barabara nimejionea hali ilivyo…kwa hakika kuna kila sababu ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa aliyenitangulia na ili kuhakikisha jitihada hizi hazirudi nyuma ni vyema ushirikiano ule mliompa yeye mhamishie kwangu nina hakika tutapiga hatua zaidi,” alisema Rufunga.  Alisema anatambua kuwa Lindi ni miongoni mwa mikoa yenye eneo kubwa kiutendaji, hivyo itakuwa ni vyema iwapo wananchi watampatia ushirikiano kutekeleza mipango iliyopo na ile itakayopangwa kwa lengo la kuijiletea maendeleo na kujikwamua katika lindi la umasikini unaowakabili wakazi wengi wa mkoa huo.  Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watendaji wote kutimiza majukumu yao kama  mikataba ya ajira zao inavyosema na kwamba hatakuwa na urafiki na mtendaji asiyetimiza majukumu yake kwa uzembe au visingizio visivyo na msingi.  “Nataka niwakumbushe watendaji wote kuwa timizeni majukumu yenu ipasavyo…najua mnajua vyema majukumu yenu sasa sitaki niwe na kazi ya kumkumbusha mtendaji juu ya hilo…jamani kama mtu umeajiriwa na serikali kufanya kazi fulani na unalipwa stahili zako na hufanyi hiyo kazi kwanini huo usiwe wizi kwa serikali na wananchi wake wanaolipa kodi zinazokupa mshahara,” alisema Rufunga.  Kabla ya Rais Jakaya Kikwete, hajamteuwa kushika nafasi hiyo ya sasa, Rufunga ambaye anamrithi Said Meck Sadick aliyehamishiwa Mkoa wa Dar es Salaam, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida na kabla ya hapo aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Newala, Masasi na Rufiji.  Mkuu huyo mpya wa Mkoa wa Lindi, alipokelewa katika kijiji cha Mitwero nje kidogo ya  Manispaa ya Lindi na wananchi, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na Serikali, chini ya uongozi wa Katibu Tawala wa Mkoa, Thomas Sowani, na kuanza ziara ya kutembelea Wilaya za Liwale, Nachingwea, Kilwa, Lindi na Ruangwa.

Chanzo - Habari Leo

No comments:

Post a Comment