Friday, August 03, 2012

Serikali kukabili changamoto ugunduzi wa Gesi

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali inajipanga kukabiliana na changamoto zinazoambatana na ugunduzi wa gesi asilia nchini na kuitaja moja ya changamoto hiyo kuwa ni ufisadi unaoweza kusababisha Watanzania wasinufaike na rasilimali hiyo.


Rais Kikwete alisema hayo jana Ikulu alipokutana na wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakiwamo wakurugenzi, wahariri wakuu, wahariri watendaji na waandishi wa habari waandamizi, ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kulihutubia taifa kila mwisho wa mwezi.

Alisema hadi sasa, Tanzania imeshagundua kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 na trilioni 28.9 ambazo zikitumika vizuri, zinaweza kubadili uchumi na maisha ya Watanzania.

Kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta nchini hivi sasa ni 18 zikiwamo zenye uzoefu mkubwa wa kufanya kazi hiyo duniani na kati ya mwaka 1954 na mwaka huu, kati ya visima 61 vilivyochimbwa, 22 vimebainika kuwa na gesi na kati ya hivyo 14 viko nchi kavu na vinane baharini.

“Changamoto nyingine ni jinsi ya kutumia mapato yatokanayo na gesi, maana tusipojipanga tunaweza kukuta kwamba mapato yetu yanaishia mikononi mwa watu wachache halafu mwishoni mwa siku wao wakaneemeka, taifa likakonda na wananchi pia wakakonda,” alisema kuongeza:

“Hivyo sisi tunasema lazima tujipange, tunaweza kuunda chombo kama gas revenue fund (mfuko wa mapato ya gesi) na tukaamua kwamba fedha zetu zitunzwe humo ili kila tunapozitumia tufahamu zimefanyia nini na zinalisaidia taifa kwa kufanya kitu gani.”

Alisema hatua hizo zisipochukuliwa, gesi inaweza kwisha halafu taifa likajikuta hakuna kitu chochote muhimu lilichofanya kutokana na mapato ya rasilimali hiyo.

Rais Kikwete alisema maandalizi mengine yanayofanywa na Serikali ni kuandaa sera ya gesi asilia, kutunga sheria ya kusimamia sekta hiyo na kurekebisha sheria iliyopo ya utafutaji wa gesi na petroli.

Alisema changamoto nyingine ambayo Serikali inajipanga kukabiliana nayo ni kuandaa wataalamu wa kusimamia sekta ya gesi katika maeneo mbalimbali, wakiwamo wa hesabu zinazohusiana na sekta hiyo, wahandisi, mafundi, wanasheria na wataalamu wa mikataba ya gesi.

Rais alisema maandalizi hayo ni muhimu na kwamba yasipofanyika, taifa linaweza kujikuta likidhulumiwa au kupunjwa mapato yanayotokana na rasilimali hiyo, au kulalamika kwamba limepunjwa hata kama halijatendewa hivyo.

Kutokana na hali hiyo, alisema wataalamu wanaandaliwa hivi sasa na taasisi kadhaa za elimu ya juu nchini zimeanzisha masomo na kozi mbalimbali zinazohusu masuala ya usimamizi wa petroli na kwamba kozi hizo zitaanza kutolewa katika mwaka ujao wa masomo.

Aliyataja maandalizi mengine kuwa ni kuanzisha kozi za ufundi mchundo katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Mtwara, ambako Wizara ya Nishati na Madini tayari imetangaza mpango wa kuwafadhili wanafunzi 50 chuoni hapo ambao watatoka mkoani Mtwara.

“Pia wizara hii ina mpango wa kusomesha wataalamu kati ya 40 na 50 kuanzia sasa na mwaka 2016 katika fani mbalimbali za masuala haya ya gesi na lengo ni kwamba tuwe tayari katika maeneo yote muhimu ya kuwa wasimamizi na kuepuka kazi zote kuchukuliwa na Wafilipino (wageni),” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alisema msingi wa kuwapata wataalamu lazima uwe endelevu, kwa kuhimiza ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati katika elimu ya msingi na sekondari.

Mgomo wa walimu
Kuhusu mgomo wa walimu, Rais Kikwete alisema Serikali inawathamini watumishi hao wa umma na kwamba kamwe haiwezi kuwadharau, isipokuwa madai yao ya sasa ni makubwa mno na “hayatekelezeki”.

“Ikiwa tutaamua kulipa kama wanavyotaka ina maana kwamba Serikali itumie kiasi cha Sh6.5 trilioni kwa ajili ya mishahara tu. Makusanyo yetu ya ndani ni Sh8 trilioni, hapo ina maana kwamba tutakuwa tunafanya kazi ya kuwalipa watumishi wa umma tu,” alisema Kikwete na kuongeza:

“Sasa tukifikia hapo hata wananchi watagoma, watasema hawa watumishi 500,000 wa Serikali wamejikusanyia hela yote ili wajinufaishe wao peke yao, kwa sababu hatutaweza kununua dawa wala kutoa huduma nyingine yoyote, itakuwa ni mishahara tu.”

Alisema Serikali inasubiri uamuzi wa Mahakama unaotarajiwa kutolewa leo na kwamba jambo linalomsikitisha ni taarifa kwamba baadhi ya walimu wamekuwa wakiwapiga na kuwatishia wenzao ambao hawakugoma.

“Mimi ninasema, kama wewe umegoma, basi siyo vizuri kwenda kum-harass (kumbugudhi) ambaye hakugoma, wale ambao wana uchungu na watoto waacheni jamani waingie darasani, wafundishe,” alisema.

Aliongeza kuwa Serikali iko tayari kuendelea na mazungumzo na walimu na kwamba anaamini kuwa kuna wakati watafikia mwafaka na kurejesha hali ya ufundishaji kama ilivyokuwa mwanzo.

Vita dhidi ya rushwa
Kadhalika, Rais Kikwete alizungumzia vita ya rushwa na kusema bado ni tatizo kubwa nchini, licha ya jitihada ambazo Serikali imefanya za kuimarisha taasisi za kupambana na tatizo hilo.

“Hii si kazi ya Serikali pekee, inahusisha taasisi zote na dhamana hii tumewapa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na huwa hatuwaingilii katika kazi yao, lakini tunasaidiana hapa na pale kuona walau tunapiga hatua,” alisema.

Kuhusu kashfa ya rada, Rais Kikwete alisema Serikali inashindwa kuwashtaki waliotuhumiwa katika suala hilo kutokana ukweli kwamba hata, Uingereza walikana Kampuni ya BAE Systems kutoa rushwa na badala yake wakasema ilikosea katika kuandika hesabu zake.

“Sasa hapo sisi tunaanzia wapi, maana kwenye asili ya tukio hili, wanasema hakuna rushwa, kwa hiyo wanasheria wetu tukiwauliza nao wanahoji kwamba tunaanzia wapi katika suala hili,” alisema.
Kuhusu kashfa ya Kagoda ambayo ni sehemu ya ufisadi wa wizi kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa), kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Rais Kikwete alisema taarifa alizonazo ni kwamba suala hilo bado linachunguzwa.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment