Tuesday, September 13, 2011

NHIF yalipa mil 478/- za huduma za afya Lindi


WATOA huduma za afya binafsi na Serikali mkoani Lindi, wamepata Sh milioni 478.3 ikiwa ni malipo ya madai yao kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 mwaka huu, imeelezwa.  

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko huo kwa Ofisi ya Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini Mtwara mwishoni mwa wiki, Meneja wa Kanda, Beatus Chijumba alisema fedha hizo ndizo walizostahili kulipwa baada ya uhakiki wa madai yao. 

Chijumba alisema kati ya hizo, Sh 274,484,346.50 zimelipwa kwa watoa huduma vituo vya Serikali, wakati watoa huduma wa vituo visivyo vya Serikali walilipwa Sh 194,883,193 na watoa huduma binafsi wa maduka ya dawa walilipwa Sh 8,960,430. 

Alisema malipo hayo ni kutokana na wanachama 42,179 waliohudhuria katika vituo vya kutolea huduma ya afya vya Serikali na wengine 19,534 waliohudhuria katika vituo visivyo vya Serikali huku waliohudhuria katika maduka binafsi ya dawa wakifikia 1,460. 

Aidha, Meneja huyo alisema katika kipindi hicho, wanachama wachangiaji waliongezeka kutoka 7,143 hadi kufikia 7,252 na hivyo kuufanya Mkoa wa Lindi kuwa na wanufaika 43,512 wanaopata huduma za afya chini ya NHIF Kanda ya Kusini. 

Chijumba alibainisha kuwa katika kipindi hicho, ofisi yake ilikusanya michango ya asilimia sita ya wanachama na waajiri wao kwa wale ambao malipo yao hayapitii Hazina moja kwa moja. 

Alisema hadi sasa mkoani humo, kuna vituo 210 vya kutolea huduma vilivyosajiliwa na Mfuko ambapo kati ya hivyo 185 ni vile vinavyomilikiwa na Serikali, 11 vya mashirika ya dini na maduka binafsi ya dawa 14. 

Hata hivyo, alisema ofisi yake inaendelea na mchakato wa kusajili vituo zaidi pamoja na maduka ya dawa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wanachama wake na hivyo kuboresha huduma.

Chanzo - Habari Leo

 

1 comment:

  1. Ni kiasi gani kati ya pesa hizi zitabaki pale Lindi kukuza uchumi? Bila shaka wenye kampuni hizi za kutoa huduma ya afya hayamilikiwi na wenyeji.

    Je, ni challenge mpya kwa sisi wanakusini kuanzisha shughuli za kibiashara zitazonufaisha Lindi na Mtwara kiuchumi? Au tuache wageni waje kuchuma na kuondoka zao kama vile dhahabu na maliasili zingine zinavyowanufaisha zaidi wazungu kuliko wa-TZ wenyewe?

    ReplyDelete