Tuesday, August 23, 2011

Wabunge wachachamaa


MBUNGE wa Kilwa Kusini, Selemani Said Bungara (CUF) jana alikuwa kivutio bungeni mjini Dodoma wakati alipozungumza kwa uchungu kuhusu kero ya maji kwa wananchi wa Kilwa Kusini na kudai kuwa, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haiwaelezi ukweli Watanzania kuhusu tatizo la maji. Mbunge huyo amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisilie kwa sababu kinajipiga chenyewe, na kisipomaliza kero ya maji kwa wananchi, mwaka 2015 wapinzani watachukua nchi. Mbunge huyo amedai kuwa, kauli ya Wizara ya Maji kuwa asilimia 57.8 ya wananchi wa vijijini wanapata maji safi ni dalili ya unafiki, na akasema kuwa CCM ni ‘longolongo’ Kwa mujibu wa Mbunge huyo, wananchi katika jimbo lake wananunua debe moja la maji kwa Sh. 500/-, hivyo hata kama mwananchi akitumia kiasi hicho kwa siku, kwa mwezi mmoja anatumia Sh. 150,000/- kwa ajili ya maji. “Aah, masikini wa Tanzania atapata wapi laki moja na nusu apate maji safi na salama” amesema Mbunge huyo na kusema kuwa takwimu za Wizara ni za uongo, kwa kuwa pengine hata asilimia 10 ya wananchi kwenye jimbo hilo hawapati maji. “Inasikitisha sana, namuomba Mheshimiwa Waziri aje Kilwa kuthibitisha kama kweli tunapata asilimia 57.8”amesema Bungara na kudai kuwa, wakati wa uchaguzi, wananchi wamekuwa wakidanganywa kwa ahadi ya kupatiwa maji. Ametoa mfano kuwa, kuna vitongoji saba Kilwa Masoko, vyote vina tatizo la maji. “Sisi wa kusini tumekosa nini, sisi watu wa kusini tumekosa nini Mheshiwa?... tunaomba Serikali ya CCM itukumbuke watu wa kusini, tunaomba Serikali ya CCM ituheshimu watu wa kusini” amesema Mbunge huyo. 


Chanzo - Habari Leo

1 comment:

  1. Kazi nzuri sana Mbunge Bungara. Wananchi wa Kusini tuko nawe sambamba na tutaendelea kuwa na wabunge na wadau wengine wote watakaonyesha kujitoa kwa mioyo yao yote kuikomboa kusini. Tunaomba uzidi kuwa mpiganaji na usikate tamaa wala kuogopa.

    Wanakusini tubadilike na ksimama kudai haki zetu! Sisi wananchi wa kusini ni watoto wa baba mmoja (Serikali hii) na wala si watoto wa kufikia!

    Ungana na wanakusini wenzio au potelea kwa wasio na mpenzi mema nasi!

    ReplyDelete