Thursday, June 28, 2012

TPDC NA BOMBA LA KUSAMBAZA GESI VIWANDANI, MAJUMBANI




Baadhi ya mabomba yatakayotumika kusambaza gesi viwandani na majumbani likiwa limetandazwa chini ya ardhi na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC). Picha na Joseph Zablon.

PEMBEZONI mwa barabara ya Mandela, jirani na eneo la biashara la Mlimani City, mafundi wanatandaza mabomba katika mrefeji uliochimbwa kutoka Ubungo mpaka katika eneo hilo.
Mabomba hayo inaelezwa kuwa ni ya kusambaza umeme wa gesi viwandani na majumbani na mpango huo unaratibiwa na kusimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC). Mpango huo wa awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.

Kukamilika kwa utandazaji wa mabomba hayo kutatoa fursa kwa Mlimani City, nyumba 57 na viwanda sita vilivyopo eneo la Mikocheni, kuanza kutumia umeme wa gesi. Mabomba hayo yatatadazwa kwenye maeneo mengine, jijini Dar es Salaam.

Gesi kusambazwa majumbani
Kulingana na ripoti ya utendaji ya TPDC ya mwaka 2011, Kampuni ya Ushauri Welekezi ya Ms. Ultimate Petroleum Technology mwaka 2007 ilikamilisha upembuzi yakinifu wa mpango wa kusambaza gesi majumbani, mahotelini na kwenye magari katika Jiji la Dar es Salaam.

Upembuzi huo umekusudia kujenga mtandao wa mabomba makubwa kando ya barabara zote za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha gesi. Pia ujenzi wa vituo 12 vya kujaza nishati hiyo katika magari.
Pia mpango huo umelenga magari 8,000 na nyumba 30,000 na gharama za mradi zinatajwa kufikia dola 55 milioni za kimarekani mpaka kumalizika kwa mpango huo. Awali walitenga dola 30 milioni kwa ajili kukamilisha mtadi huo.

Kuanzia mwaka jana mpaka sasa viwanda 35 zikiwamo nyumba 17 ambazo zipo kwenye mradi wa majaribio vinatumia nishati hiyo.

Kutokana na kampuni hizo zimeokoa dola 187 milioni za kimarekani baada ya mwaka jana kuanza kutumia gesi.

"Fedha hizo zingetumika iwapo wangetumia mafuta ya petroli na dizeli" inasema sehemu ya taarifa ya TPDC ya utekelezaji wa mradi huo.
Tangu mwaka 2004 mpaka mwaka jana Serikali imepata Sh114 milioni kutokana na mauzo ya gesi.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa kusudio la matumizi ya umeme wa gesi ni kupunguza matumizi ya nishati asili kwa mfano, mkaa, kuni na mafuta mengine yanayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya nishati. Umeme unaozalishwa na gesi asilia ni megawati 341.

Pia ripoti hiyo inabainisha kwamba hivi sasa mabomba yanatandazwa kwa ajili ya kusambaza gesi katika eneo la biashara la Mlimani City na maeneo ya jirani.

Baada ya mpango huo kukamilika kutakuwapo na ongezeko la watumiaji wa umeme utokanao na gesi.
"Hivi sasa Serikali inaweka mkazo katika uzalishaji wa umeme wa gesi kuliko ule wa maji (hydropower)" inasema taarifa hiyo.

Mahotelini ni kati ya maeneo ambako umeme wa nishati ya gesi asili, utasambazwa.
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, John Ngeleja anasema mpango huo ulianza kutekelezwa jijini Dar es Salaam kutokana na jiji hilo kuwa na mahitaji makubwa ya umeme kuliko miji mingine Tanzania.
Pia mpango umetekelezwa Dar es Salaam kwa sababu maeneo yake, yamepimwa na kuacha nafasi ya kupitisha mabomba hayo kwa ajili ya mradi huo.
Mpango huo utasambazwa Mkoa ya Lindi ambako gesi hiyo inazalishwa kadiri mradi utakavyozidi kupanuka.

Ofisa Mtafiti katika Kurugenzi ya Masoko na Uwekezaji, Emmanuel Gilbert anasema mradi wa kutandaza mabomba ni tofauti na ule wa majaribio ambao unatekelezwa hivi sasa katika nyumba 17 za wafanyakazi wa TPDC Mikocheni na katika viwanda 35 kikiwamo cha Saruji cha Twiga, kilichopo eneo la Wazo.

Anayataja maeneo ambayo yapo katika awamu ya pili ya mradi huo ni Chuo cha Maji Rwegarulila hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam.
Mabomba mengine anasema yatafungwa katika matoleo yaliyopo kona ya kuelekea eneo la Sinza kutoka barabara ya Sam Nojuma na katika makutano ya Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma kwa ajili ya Kambi ya Jeshi Wananchi Lugalo na watu wanaoishi kambini humo.

Umeme wa uhakika kupatikana
Gesi ya asili ilianza kuzalisha umeme Julai 2004, katika mitambo ya Shirika la Ugavi Nchini (Tanesco) Ubungo. Katika mpango huo walianza kuzalisha megawati 151 na mpaka sasa nyumba 17 pekee zinatumia nishati hiyo kwa majaribio katika eneo la Mikocheni.
Gilbert anasema lengo la mradi ni kupunguza umeme wa maji ambao siyo wa uhakika kutokana na uhaba wa mvua na kwamba mpango huo utawawezesha kupata umeme kwa bei ya chini tofauti na sasa.
Pia mradi umelenga kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa. Takwimu za Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), zinabainisha kwamba zaidi ya magunia 40,000 ya mkaa yanatumika kila siku katika Jiji la Dar es Saalam.
Kiwango hicho ni tofauti na kile ambacho kinatumika mikoa mingine nchini na kiasi cha mkaa ni tofauti na nishati ya umeme na nchini kwani kwa siku megawati 850 zinahitajika kuzalisha umeme.
Wakati mwingine megawati hizo zinashuka na kufikia megawati 600 na kusababisha mgawo wa umeme nchini kutokana upungufu wa maji katika mitambo ya kuzalishia umeme inayotumia mvua.
Pia mradi huo unatarajiwa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununua aina nyingine za gesi na mafuta kutoka nje ya nchi.
Umeme wa gesi asili unatarajiwa kupunguza uharibifu wa misitu na uchafuzi wa mazingira.

Ofisa huyo anasema mpango huo umelenga kujenga mtandao wa mabomba makubwa kando ya barabara zote za Jiji la Dar es Salaam na ujenzi wa vituo vitatu vya kushindilia gesi katika mitungi, vituo 12 vya kujaza gesi kwenye magari.

Anasema mradi huo utagharimu dola 55 milioni za Marekani mpaka utakapokamilika. Fedha hizo ni pamoja na vyanzo vingine pia zinatokana na gawio la asilimia 50 ya mauzo ya gesi nchini kutoka serikalini.

Gilbert anasema ujenzi wa bomba la kilometa saba kutoka Ubungo hadi Mikocheni upo katika hatua nzuri na kituo cha gesi kilichopo katika hoteli ya Serena ambacho kinasambaza katika hoteli zingine pia na cha Ubungo vinatoa tija. Anasema bomba la Ubungo lina ukubwa kutosha kulingana na mahitaji ya baadae ya nishati hiyo kwa wateja. Anasema baada ya bomba lingine la Mtwara mpaka Dar es Salaam kukamilika litaongeza usambazaji wa nishati hiyo kwa watumiaji.

Vituo vya kuuzia gesi
Gilbert anasema watumiaji wa gesi watakuwa wakilipia huduma hiyo kwa Luku. Wakazi watafungiwa mashine na kununua uniti katika vituo vilivyokusudiwa.

Bei ya kuuzia gesi ipangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Gesi (Ewura) na kwamba nishati hiyo ya umeme inauzwa kwa bei ya chini kuliko nyingine nchini.

Pia umeme huo ni rahisi kuliko mwingine na kwamba bei ya kuuza umeme huo umepangwa sawa na bei ya kipimo cha kopo la mkaa na kutoa punguzo la asilimia 20 kwa bei iliyopo sokoni.
"TPDC ni chombo cha Serikali hivyo bei zake tumekokotoa kwa kuwianisha na bei za nishati zingine ambazo zinatumiwa na wananchi wengi ambazo ni kuni na mkaa," anasema.

Habari na Joseph Zablon
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment