Friday, December 02, 2011

Mbunge CUF ‘aibeba’ CCM

MBUNGE wa Lindi Mjini, Salum Barwani (CUF) a m e s e m a anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/15 kwa kuwa chama chake hakikushinda uchaguzi mkuu wa urais.  Barwani alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili ofisi kwake baada ya kuwasili jimboni  kutoka kwenye Mkutano wa Bunge mjini Dodoma.  Aliwataka wananchi wa jimbo lake kutambua kuwa maendeleo hayaji kwa miujiza, wala juhudi zake peke yake, ila yatakuja baada ya kuwa na mshikamano wa pamoja kati ya Serikali ya CCM,  wananchi na yeye.  “Ndugu zangu maendeleo ya Lindi hayawezi kupatikana kwa juhudi za mbunge peke yake, bali umoja na mshikamano ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo, mimi peke yangu siwezi kuleta  maendeleo kama mnafikiria hivyo basi ni ndoto ya mchana,” alisema.
  Mbunge huyo pia alikiri kuwekwa ‘kiti moto’ na baadhi ya wananchi aliokutana nao wakimtuhumu kukaa muda mrefu Dar es Salaam bila kwenda kuwaona.  Mbunge huyo alisema Baraza la Utendaji la Wilaya la CUF lilimwita na kumweka kikao  Jumamosi na kumhoji sababu za kutumia muda mwingi Dar es Salaam na kutokwenda kuona  wananchi baada ya Bunge la Bajeti.  Alisema Kamati hiyo ilitaka kujua uhalali wa kukaa muda mrefu nje ya jimbo kwa kuwa vikao  vya Bunge kwa mwaka hufanyika mara nne tu.  Katika kikao hicho, Barwani alisema alijitetea kuwa licha ya vikao vya Bunge alivyokuwa akihudhuria Dar es Salaam, bado kuna kazi zingine za ufuatiliaji wa ahadi za Serikali kwenye ofisi za idara na wizara, baada ya kukamilika kwa vikao vya Bunge.  Barwani aliendelea kujitetea kuwa yeye bado anasoma utendaji wa kazi za Bunge kwa hiyo  anapaswa kufahamu zaidi kwa kuwa bungeni.  Wajumbe hao pia walimwuliza kuhusu mpango aliowaahidi wa maji, baada ya kutoka ziarani China na Ujerumani.  Alijitetea kuwa mpango huo bado upo hata kama muda uliopangwa kukamilika kama  alivyoahidi umepita.  Alisema alipata mashine za kuchimba visima virefu vya futi 60, lakini wataalamu walimwambia kuwa maji yako kina kirefu zaidi na inahitajika mashine yenye uwezo wa kuchimba kisima cha futi 120.  Mbunge huyo alisema mashine moja ni Sh. milioni 40 ambazo wafadhili walishapatikana  kwa hiyo Januari itapatikana na mradi utaanza.  Kuhusu elimu, aliahidi kutoa msaada wa madawati 100 kwa shule za msingi na vitabu 2,800 vya masomo mbalimbali kwa wanafunzi sekondari za Manispaa ya Lindi.  Katika msaada huo, Barwani aliahidi kutoa madawati hayo yenye thamani ya Sh milioni 4  kwa shule za msingi na vitabu 2,800 vyenye thamani ya Sh milioni 7 vya Sayansi, Jiografia,  Fasihi na Hisabati kwa sekondari.  Barwani alisema shule nyingi za msingi na sekondari kwa kipindi kirefu zinakabiliwa na  upungufu wa vitendea kazi kama vile vifaa vya kujifunzia na kufundishia, madawati na nyumba  za walimu.  Alisema ameamua kuanza na hayo, huku matatizo mengine akiendelea kuyatafutia ufumbuzi  ikiwa ni pamoja na kutafuta wafadhili wa nje na ndani.  Sambamba na hilo, pia alitoa baiskeli za watu wenye ulemavu 50 zenye thamani ya Sh milioni  tatu.  Mbunge huyo aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kumpa ushirikano wakati huu mgumu ili  atekeleze majukumu yake.

Chanzo - Habari Leo

No comments:

Post a Comment