Thursday, December 08, 2011

Jumuiya ya Uingereza yasaidia Sh 100 milioni Elimu Masasi

JUMUIYA ya African Palms ya nchini Uingereza imetoa Sh 100.6 milioni kwa ajili ya kusaidia ukuzaji elimu katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara.Fedha hizo ambazo zimetolewa kupitia uchangiaji wa mfuko wa elimu wa Mamlaka ya Elimu nchini (Tea) ikiwa na lengo la kuinua elimu katika wilaya hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mchungaji Tabolt mstaafu wa Kanisa la Anglikana ambaye aliendesha huduma ya kiroho wilayani humo, alisema ameamua kuisaidia Masasi kwani ameishi katika mazingira hayo na anaijua hali ya elimu iliyopo katika eneo hilo.

“Nimeishi huko kwa muda mrefu nimeona shida na haja ya wakazi wake katika sekta ya elimu, mchango huu utasaidia kukuza uelewa wa watoto wengi zaidi, na hii itasaidia kuleta maendeleo wilayani humo,” alisema Mchungaji Tabolt.

Alisema watoto wanapaswa kufurahi na kuchangamka hivyo baadhi ya fedha zitatumika kununulia vifaa vya michezo.Naye Meneja Habari, Elimu na Mawasiliano wa Tea, Sylivia Lupembe alisema wamekuwa wakipokea msaada huo kutoka kwa mdhamini huyo kwa muda wa miaka mitatu sasa.

Alisema msaada huu unatokana na asasi moja iliyoanzishwa na mchungaji huyo ya kuuza minyaa kutoka huko Masasi ijulikanayo kama African Palms Association ambayo baada ya mauzo faida inarudi kusaidia elimu wilayani humo.

“Tumenunua vitabu 16,529 vya ngazi ya kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba ,pia tumeweza kununua vifaa vingine vya michezo kwa ajili ya wanafunzi hao”, alisema Lupembe.Alieleza kuwa zaidi ya shule 153 wilayani humo zimenufaika na vitabu hivyo, na wanafunzi wengi wamefaidika kupitia msaada huo, jambo linalokuza elimu yetu.

Chanzo: Mwananchi Newspaper, Wednesday, 07 December 2011

No comments:

Post a Comment