Monday, September 19, 2011

CHF kuwashika mkono wa afya njema yatima wa Lindi

WATOTO yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu mkoani Lindi, watapata kadi za matibabu ili kuwawezesha huduma za Mfuko wa Afya kwa kipindi cha mwaka mzima.  Taarifa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ambao ni wasimamizi wa huduma za Mfuko wa Afya Jamii (CHF) zimesema kuwa jumla ya watoto 1,000 kutoka halmashauri ya Wilaya ya Lindi na Kilwa ni kundi la awali la wanufaika hao.  Akiongea kwa njia ya simu na gazeti hili, Ofisa anayeshughulikia huduma za CHF ndani ya Bima ya Afya , Rehani Athumani amesema hafla hiyo itafanyika mkoani Lindi na Mgeni Rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mecky Sadik ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Rehani amesema, tayari timu ya viongozi waandamizi wa NHIF wakiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu Hamisi Mdee wako mkoani humo kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi huo na kufanya tathmini ya huduma za mfuko wa Afya ya jamii mkoani humo. 
Kuhusu huduma za matibabu kwa watoto hao, Rehani amesema huduma hizo watakazopata watoto hao zitawawezesha wao na walezi wao katika familia kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima. Ameongeza kuwa sanjari na mchango huo Serikali Kuu pia itachangia juhudi hizo kwa kutoa fedha nyingine zijulikanazo kama fedha za “tele kwa tele” ili kufanya huduma za matibabu ziweze kupatikana kwa urahisi ,hasa huduma za dawa ambazo ndio kilio kikubwa cha wananchi na wanachama wa CHF. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2011 Mfuko wa Afya ya Jamii ulikuwa unahudumia wanufaika milioni 3.3 katika Halmashauri mbalimbali nchini huku wanufaika 79,314 wakiwa ni kutoka  mkoani Lindi.  Mfuko wa CHF ndio unaohudumia wananchi wengi zaidi ukilinganisha na Mifuko mingine ya huduma hapa nchini.  Uchangiaji katika Mfuko huu kwa mujibu wa Rehani ni kati ya Sh elfu tano hadi Sh elfu 15 kwa mwaka na huduma za matibabu ni kwa mwaka mzima kwa Kaya ambayo inajumuisha Baba, Mama na watoto chini ya miaka 18.

Chanzo - Habari Leo

No comments:

Post a Comment