Monday, August 22, 2011

JK: Viongozi tafuteni majibu ya matatizo ya wananchi

Amesema kila kiongozi kwa ngazi yake anao wajibu wa kukabiliana na kumaliza matatizo na kero za wananchi walio chini yake badala ya kusubiri uongozi wa juu yake kufanya kazi hiyo. Rais Jakaya Kikwete, amewaambia viongozi kuwa kazi yao kubwa ni kusikiliza na kutafuta majawabu ya matatizo na kero za wananchi kwa kuwa uongozi ni utumishi wa wananchi.   Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi jioni alipozungumza na viongozi wa Mkoa wa Lindi baada ya kula nao futari mjini Lindi. Aidha, alitumia fursa hiyo kufahamu hali ya tatizo la maji linaloukabili mji wa Lindi. Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Lindi. Rais Kikwete alielezea umuhimu wa viongozi kutimiza wajibu wao baada ya kuwa amejulishwa kwamba moja ya sababu ya kukosekana kwa maji ya kutosha katika mji wa Lindi ni kukosa Sh. milioni 25 za kununulia mafuta ya dizeli kwa ajili kuendeshea mitambo ya umeme kwenye chanzo cha maji Kijiji cha Kitunda. 
Rais Kikwete aliwahoji viongozi wa Mkoa wa Lindi likiwamo Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mamlaka ya Maji la Mji wa Lindi (Luwasa), Halmashauri ya Mji wa Lindi na ule wa Mkoa kwa kushindwa kutafuta kiasi hicho cha fedha ili kuwapatia wananchi maji. Aliagiza ngazi mbalimbali za Mkoa wa Lindi kukutana leo kuhakikisha kuwa dizeli inapatikana kuwezesha mitambo ya Kitunda inafanya kazi. Aidha, jana Rais Kikwete alitembelea chanzo cha maji cha Mji wa Lindi kilichopo katika Kijiji cha Kitunda, Kata ya Msinjahili. Akiwa hapo, Rais alielezwa hali ya upatikanaji maji kutoka katika chanzo hicho na kujionea hali halisi ya mitambo. Kwenye chanzo hicho cha maji cha Kitunda, Rais Kikwete alionyeshwa mashine mbili za kusukuma maji na akakagua visima viwili vikubwa ambako huvutwa maji na baadaye kuzungumza na wananchi wa eneo hilo. Alielezwa kuwa upatikanaji maji katika Mji wa Lindi si mzuri kwa kuwa hadi Julai, mwaka huu, ni lita 550,000 tu za maji zilizokuwa zinawafikia wakazi 92,000 wa mji huo kwa siku sawa na asilimia 11 tu ya mahitaji. Rais Kikwete aliambiwa kuwa Mji wa Lindi unahitaji lita milioni tatu za maji kwa siku. Akizungumza na wananchi wa Kitunda, Rais Kikwete, aliwaambia viongozi wa Mkoa wa Lindi kuhakikisha kuwa wakazi wa kijiji hicho pia wanapata maji kutokana na chanzo hicho cha maji.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment