
SERIKALI imesaini mkataba wa ubia na Kampuni ya Sichuan Hongda ya China, wa kuendesha mradi wa kuchimba chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga utakaogharimu Sh4.8 trilioni. Katika mkataba huo uliosainiwa Dar es Salaam jana kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), miradi hiyo inatarajiwa kuanza kufanyiwa kazi ndani ya kipindi cha miezi sita na 36 ijayo. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami alisema NDC na Hongda, zimeunda kampuni nyingine kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kiasi hicho cha fedha kinapatikana. “Taarifa kutoka China zinasema kwamba kampuni hii tayari ina Dola za Marekani 600 milioni ambazo zinaweza kuanza na mradi huu, nyingine zilizobaki zitatafutwa ili kukamilisha mradi ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya Tanzania,” alisema Chami. Chami alisema mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili; uchimbaji wa chuma na uchimbaji wa makaa ya mawe kwa ajili ya uzalishaji wa megawati 600 za umeme. Alisema katika mradi huo uliopo wilayani Ludewa mkoani Iringa, Serikali inaanza kwa kumiliki asilimia 20 za hisa lakini kampuni hiyo ikisharudisha fedha zake za uwekezaji, Serikali inaweza kununua hadi asimilia 49 za hisa hizo. Alisema kuwa baada ya miezi 36 uchimbaji wa chuma ndipo, utaanza katika eneo hilo na kufafanua kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe, utaanza baada ya miezi sita, baada ya kampuni hiyo ya China kukamilisha uchunguzi wake katika eneo la Mchuchuma. “Uchunguzi unaonyesha kuwa eneo la Mchuchuma lina tani 483 milioni za makaa ya mawe ambayo tunaweza kuyatumia kwa zaidi ya miaka 500 ijayo. Huu umeme wa megawati 600 utazalishwa kwa awamu, kila awamu itakuwa ikizalisha megawati 150,” alisema Dk Chami. Alisema kuwa Serikali imeikabidhi wizara yake jukumu la kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika kutegemea uchumi wa kilimo na kujikita katika uchumi wa viwanda. Akisema mpango huo utaanza na kufanikiwa ifikapo mwaka 2025. “Mradi huu kwa kiasi kikubwa utatatua tatizo la umeme, tumeamua kuanza na mradi wa makaa ya mawe kwa ajili ya uzalishaji wa umeme ili kuendesha viwanda kwa kuwa uzalishaji wa chuma unahitaji megawati 300, zilizobaki zitaingizwa katika gridi ya taifa” alisema na kuongeza: “Mradi huu utasaidia kuongeza ajira, kukua kwa uchumi na kusaidia kukua kwa miradi mingine hasa ya viwanda kutokana na upatikanaji wa umeme na chuma.” Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo, alisema mradi huo una mafanikio makubwa na ni ukombozi wa uchumi kwa Tanzania. “Huku ni kuelekea kujenga msingi kwa ajili ya kusonga mbele kwa awamu ya pili ya ukombozi wetu, ukombozi wa kiuchumi.
Natoa shukrani zangu kwa uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria ambao faida yake tumeiona kwa NDC na Hongda,” alisema Dk Bilal, “Ukombozi huu sasa utaifanya Tanzania kuwa na maendeleo ya viwanda kama ilivyo kwa baadhi ya nchi jirani.” Mzindakaya atema cheche Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NDC, Chrisant Mzindakaya alisema kuwa upungufu utakaojitokeza katika mradi huo ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), utapaswa kuelekezwa katika bodi hiyo. “Nina uzoefu wa miaka 44 katika siasa na uongozi. Nchi hii naifahamu vizuri, Wapo watanzania hodari wa kuzuia wenzao kusonga mbele, napenda kuwaeleza kuwa hakuna mwenye ubavu wa kuzuia mradi huu usisonge mbele, lolote litakalotokea tutabeba lawama,” alisema Mzindakaya. Alisema kuwa mkataba huo siyo Biblia wala Msahafu, akisisitiza kwamba lengo la NDC ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2018, nchi iweze kuzalisha megawati 1,800 za umeme. Mbunge alalamika . Akizungumza pembeni baada ya hafla hiyo, Mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe alisema wakati Tanzania ikifikisha miaka 50 ya uhuru, wananchi wa Ludewa bado hawajapata uhuru. “Uhuru utafika Ludewa iwapo umeme huu utazalishwa na kuwafikia wananchi, uhuru utakamilika kwa asilimia 100 kama barabara zitajengwa kwa kiwango cha kuridhisha,” alisema Filikunjombe. Kampuni ya Sichuan Hongda ilishinda kampuni nyingine 48 zilizotaka zabuni ya kusimamia mradi huo ambao ulilenga kupata kampuni moja itakayoweza kuchimba kwa pamoja makaa ya mawe na chuma.Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment