Kisiwa cha Songosongo kinachoneemeka na mradi wa gesi
Friday, 03 February 2012 13:27
Msimamizi wa ujenzi wa kisiwa kipya cha kuzalisha gesi katika kisiwa cha songosongo,Craig Kelly akitoa maelezo kwa waandishi wa habari waliotembelae madi houhivi karibuni
Na
Boniface Meena
KATIKA hali ya kawaida ni nadra sana hapa nchini kukuta jamii ambayo inapata umeme bure, maji bure, elimu bure bila kulipa gharama zozote.
Yumkini kupata umeme ni ngekewa katika jamii ya kitanzania ambayo ni asilimia 15 tu kati ya watu milioni 40 ndiyo inayopata umeme.
Na ni nasibu kubwa zaidi kwa sasa ambapo gharama hizo zimepandishwa hadi kufikia asilimia 40.29.
Pamoja na kuwa hali hiyo si ya kawaida hapa nchini neema hiyo ipo katika kisiwa cha Songosongo kwa wananchi wake ambao hupata huduma hizo bure kutokana na mradi wa gesi ya Songosongo.
Mradi huo umeweza kusaidia maisha ya wananchi hao kuwa ya gharama za chini kwa wao kujitafutia mahitaji mengine ya kujikimu.
Meneja Mkuu Msaidizi wa PanAfrica Energy ambao ndiyo wanaoendesha mradi wa gesi Songosongo, William Chiume anasema kuwa wameweza kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwa mradi huo uko eneo lao na unahitaji kuwanufaisha kwa namna moja au nyingine.
Chiume anasema kuwa mradi umeweza kusaidia kampuni yao kujenga madarasa mawili ya shule ya awali ambayo na vifaa vyote vinavyohitajika kwa shule hiyo hivyo kuwasaidia watoto wote wa Songosongo kuweza kusoma katika madarasa hayo.
'Tumetumia kiasi cha shilingi milioni 80 katika madarasa haya na vifaa vilivyomo ili kuweza kuwaingiza watoto hawa wadogo katika elimu ya awali,'anasema Chiume.
Anasema kuwa wameweza kutoa huduma ya umeme bure kutokana na gesi wanayochimba ikiwa ni pamoja na kutengeneza mtandao wa maji kwa eneo zima baada ya kuyatengeneza na kuyaondoa chumvi ili yaweze kunyweka na kupikia.
Kuhusu kutoa ufadhili kwa wanafunzi kusoma sekondari jijini Dar es Salaam, anasema kuwa hutumia kiasi cha Sh 15 milioni kila mwaka kuwasomesha wanafunzi 20 wanaofanikiwa kuingia sekondari kutoka Songosongo shule ya msingi.
Anasema hiyo imeweza kuwasaidia wanafunzi hao kuwasaidia wazazia wao kifedha na kuboresha maisha ya kisiwa cha Songosongo.
Anasema kuwa hivi sasa kampuni yake inamiliki visima sita vya gesi katika eneo hilo ambavyo asilimia 80 ya gesi yake hutumika katika uzalishaji wa umeme na asilimia 15 viwandani.
Pamoja na neema hizo, kisiwa cha Songosongo bado kina changamoto.
Viongozi wa hapa wanazitaja changamoto ambazo zinawakabili haswa katika sekta ya afya kutokana na kukosekana kwa madaktari katika hospitali yao ambayo imekuwa ikisimamiwa na wauguzi wasaidizi.
Diwani wa Kata ya Songosongo iliyopo katika Mkoa wa Lindi, Hassan Yusuph anasema kuwa mradi wa gesi Songosongo umefanya ipige hatua kutokana na kutoa kipaumbele katika mambo ya jamii.
'Huduma za jamii hapa kwetu ni za uhakika kama shule, maji, umeme na vyote tunapata bure na kama umeme haujawahi kukatika hivyo tunajivunia hali hii,'anasema Yusuph.
Anasema kisiwa hicho ambacho kina wakazi zaidi ya 7000 kimekuwa kikikabiliwa na changamoto kubwa ya kubadilisha namna ya kuishi tangu mradi huo wa gesi uingine kisiwani hapo.
'Wananchi wanakabiliwa na namna ya kubadilisha maisha yao hasa katika elimu ili waweze kufanya kazi zinazofanywa na wageni wanaokuja Songosongo,'anasema.
Yusuph anasema kuwa kazi kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni uvuvi lakini hivi sasa vijana wengi ambao walikuwa wakijiingiza kwenye kazi hiyo wameanza kukimbilia shuleni kutokana elimu kuboreshwa na kuahidiwa nafasi za kusomeshwa sekondari mara wanapofaulu.
'Hatuna shule ya Sekondari hapa lakini wanaoendesha mradi wa Songosongo wametoa nafasi kwa wanafunzi 20 kila mwaka kwenda shule ya sekondari Makongo jijini Dar es Salaam kusoma mara wanapofaulu,'anasema na kuongeza;
'Hii imewapa changamoto kubwa kwa kuwa kila anayesoma anawaza nafasi hiyo asiikose na inatusaidia kwa kweli.'
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Songosongo, Mohammed Mwalimu anasema kuwa shule hiyo imekumbwa na changamoto ya wanafunzi wengi kutaka kusoma hivi sasa lakini kuna uhaba wa waalimu.
Anasema hivi sasa wako waalimu watatu na wanahitajika waalimu tisa ili iweze kuwasaidia wanafunzi hao ambao ongezeko lao limekuwa kwa kasi.
Kwa upande wa kituo cha afya cha Songosongo, muunguzi msaidizi ambaye ndiye anayesimamia kituo hicho, Matha Robert anasema kuwa kituo kiko katika hali nzuri na kinatoa huduma zote lakini kuna upungufu wa madaktari na wauguzi.
Anasema kuwa wanahitaji madaktari wawili na muuguzi mmoja ambao wataweza kushughulikia matatizo makubwa ambayo yanawakabili wagonjwa wanaofika hapo na kukosa matibabu.
'Kuna mambo ambayo yanatushinda hivyo huwa tunawakimbiza wagonjwa Kilwa Masoko kwa kutumia boti ya kasi ya kampuni ya PanAfrica Energy wanaoendesha mradi wa gesi wa Songosongo,'anasema Matha.
Mradi wa kuzalisha gesi ya songosongo ulianzishwa mwaka 2004.
Mradi huo umeweza kuokoa gharama za uzalishaji kiasi cha dola za kimarekani, bilioni 1.8.
Si hivyo tu, bali mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotumia gharama ndogo za uzalishaji kwa afrika mashariki, kiasi cha Tsh 65 kwa unii moja.
Hata hiyo pamoja na kuwepo kwa mradi huo wa kuzalisha umeme, bado kiwango cha umeme hapa Tanzania ni kidogo ukilinganisha na majirani zetu wa Kenya na Uganda.
Inasadikiwa kuwa, ni asilimia 15 pekee ya watanzania ndiyo wanaopata nishati hii, na wanaobaki hulazimika kutumia kuni, mkaa, na mafuta ya taa kwa matumizi ya kiuchumi na kijamii.
Pasipo Songosongo, serikali ingelazimika kutumia gharama kubwa zaidi kuzalisha umeme.
Serikali haina budi kutafuta njia mbadala za kuzalisha umeme. Nishati hii ikipatikana kwa urahisi na unafuu, itakuwa ni chepuo kwa kwa kuleta maendeleo ya taifa na kwa mtu mmoja mmoja.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment