HALMASHAURI ya manispaa ya Lindi, imetumia zaidi ya Sh4 bilioni kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha Julai 2010 hadi Juni 30 mwaka 2011. Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ahmad Sawa , wakati akitoa taarifa za mapato na matumizi kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa DDC mjini humo jana. Sawa, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 Halmashauri ya Manispaa hiyo ilikadiriwa kukusanya Sh7.6 bilioni kutoka kwenye vyanzo vya ndani na ruzuku ya serikali kuu, hadi kufikia Juni 30, 2011, lakini kutokana na matatizo mbalimbali imeshindwa kufikia lengo la kufanikiwa kukusanya Sh5.2 bilioni sawa na asilimia 79.46. Aidha Mkurugenzi wa Manispaa huyo alisema kuwa, halmashauri ilikadiria makusanyo ya ndani yatakuwa Sh5.2 bilioni na kufanikiwa kukusanya Sh4 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 87, na makusanyo kutoka Serikali kuu ilikadiriwa kuwa Sh4.2 bilioni ikiwa ni asilimia 72.34. Sawa alisema kwa kipindi hicho halmashauri hiyo imetumia Sh4.9 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 65 ikiwa fedha kutoka mfuko wa vyanzo vya ndani . Alisema kuwa jumla ya Sh3.3 bilioni fedha za ruzuku kutoka serikali kuu zimetumika ikiwa ni sawa na asilimia 84.58, huku mapato kutoka kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo imetumia Sh1.2 bilioni sawa na asilimia 60.08 na kufanya jumla kuu ya matumizi hayo kuwa ni Sh4.9 milioni sawa na asilimia 65 ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye manispaa hiyo. Sawa alisema mapato ya ndani yanaendelea kuongezeka na kuimarika kutoka Sh3.8 bilioni katika kipindi cha mwaka 2008/09 hadi kufikia Sh5.6 bilioni kwa mwaka 2009/10 ikiwa ni ongezeko la Sh1.8 bilioni sawa na asilimia 32. Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/12 mapato ya ndani yataendelea kuimarika kwa kuwa kuna ongezeko la kata tano zenye vyanzo vizuri vya mapato zilizohamishwa kutoka wilaya ya Lindi kuingia manispaa hiyo.
Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment