Sunday, September 25, 2011

Mkuchika ataka elimu isadie vijana kujiajiri

WADAU wa elimu nchini, wametakiwa kutoa elimu itakayowawezesha vijana kujiajiri na kumudu ushindani katika soko la ajira ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wito huo ulitolewa wiki iliyopita  jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi  katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Mkuchika,  katika hotuba yake kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Maadhimisho hayo yalikuwa yameandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF).Mkuchika alisema elimu inayotolewa sasa kwa vijana katika ngazi mbalimbali chini hajasaidia kuwaondoa vijana katika mazingira magumu ya kuishi.Alisema hali hiyo inachangiwa na elimu hiyo kuwajengea vijana dhana ya kufikiria zaidi  kuajiriwa badala ya kujiajiri. “Elimu yetu lazima ifike mahala ambapo wahitimu watafikiria kujiajiri wenyewe ili kuleta maendeleo yao na kukuza uchumi wa taifa kwa jumla, kwa hiyo ni vizuri vijana wakafundishwa kuelewa namna ya kujiajiri na kutotegemea kuajiriwa,”alisema.
Waziri huyo alisema kama Tanzania haitajikita katika mafunzo yanayolingana na kipindi hiki cha mpito,  Watanzania watabaki kuwa wasindikizaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Pia alisema idadi ya wasomi nchini imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na ongezeko la shule na  vyuo, hivyo kusababisha wahitimu wengi kukosa ajira na kwamba ni vigumu wote kuajiriwa na serikali. Katika hatua nyingine, Mkuchika aliwataka Watanzania kujituma katika kufanyakazi, ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Dk Evans Rweikiza, alisema sekta binafsi inakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa rasilimali watu  Alisema mataifa tajiri, hayana utajiri kama Tanzania na kwamba lakini yameendelea kwa sababu yamewekeza katika rasilimali watu.  “Sekta nyingi binafsi zinapenda kuajiri watu kutoka nje ya nchi au waliopata elimu zao huko kwa sababu hata utendaji kazi wao ni tofauti na wahitimu wengi hapa nchini, kama unavyojua wanataka kuona mtu anazalisha zaidi ili wapate faida,”alisema Dk Rweikiza.

Chanzo - Mwananchi

No comments:

Post a Comment