Wednesday, October 05, 2011

Sekondari ya Ndwika yatimiza miaka 100

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 100 za shule kongwe ya Sekondari ya Wasichana ya Ndwika iliyopo Lulindi, Masasi mkoani Mtwara. Mkuu wa shule hiyo ya bweni, Aluna Bakari alitoa taarifa hiyo alipokuwa anazungumzia maandalizi ya sherehe hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.  “Tunamshukuru Spika Makinda kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe zetu za kihistoria zinakazokwenda sambamba na harambee ya kukamilisha miradi kadhaa kwa ajili ya ustawi wa elimu shuleni na jamii inayotuzunguka,” alisema Bakari. Alisema kwamba uongozi wa shule hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 360 una kila sababu za kuadhimisha miaka 100 ya shule hiyo kutokana na mchango mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii, hasa kwa watoto wa kike. “Hiki si kitu kidogo, tuna kila sababu za kuwaenzi waasisi wa shule, ndiyo maana tumeandaa sherehe hizi. Miaka 100 ya kumpa elimu mtoto wa kike si mzaha, lazima tujipongeze na kuweka mikakati zaidi ya kuwakomboa wanawake kielimu,” alisema. Alimpongeza Spika Makinda ambaye kati ya mwaka 1965 na 1968 alipata elimu ya Sekondari katika shule ya Wasichana Masasi.
Mkuu huyo wa shule amewataka wadau, wakiwamo watu waliowahi kusoma kufanya kazi au kuwa karibu na taasisi hiyo na wakereketwa wa maendeleo ya elimu nchini kujitokeza kusaidia kufanikisha sherehe hiyo, ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa kituo cha maarifa shuleni hapo. Mbali ya fedha, aliitaja michango mingine inayokaribishwa kutoka kwa wadau mbalimbali kuwa ni pamoja na saruji, mabati na ushauri. Aliwaomba walio mbali na wenye nia ya kuchangia kuwa wanaweza kupitishia kwenye akaunti ya maendeleo ya shule yenye namba 705 120 0111 katika Benki ya NMB tawi la Masasi. Sekondari ya Ndwika ilianzishwa na Kanisa la Anglikana kupitia shirika lake la UMCA na ilikabidhiwa kwa serikali mwaka 1970 ikiwa chini ya mkuu wa kwanza wa shule mzalendo, Magdalena Sonje. Ilipoanzishwa ilikuwa chini ya Janeth Dalton, raia wa Uingereza. Miongoni mwa waliosoma katika shule hiyo ni Thecla Mchauru, mmoja wa wauguzi na walimu wa kwanza wa kike nchini ambaye baadaye alishika nyadhifa kadhaa katika chama na Serikali, akiwa pia mmoja wa watu waliokuwa washauri wa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mbunge wa sasa wa Masasi, Mariam Kasembe pia alisoma shuleni hapo.
Chanzo - Habari Leo

No comments:

Post a Comment