MBUNGE wa Jimbo la Lindi Mjini, Salum Baruany - pichani amewashauri watu waliowahi
kusoma katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania kushirikiana katika kufanikisha tamasha la
kuchangia maendeleo ya elimu kwa ajili ya mikoa hiyo. Baruany aliyasema hayo juzi katika
kikao cha maandalizi ya tamasha la kuchangia maendeleo ya elimu kwa mikoa ya Lindi,
Mtwara na Ruvuma kilichofanyika Ukumbi wa Imasco, Temeke jijini Dar es Salaam. Akiwa
mmoja wa waalikwa wa vikao hivyo vya kila wiki, Baruany alielezea kukunwa kwake na
ubunifu wa baadhi ya wanafunzi walioamua kuwahamasisha wenzao kukumbuka walikotoka
kielimu, kwa lengo la kuwainua wengine. “Nawapongeza sana. Ni wachache wanaoweza
kukumbuka walikotoka, hasa kielimu. Hapa mmelenga, mikoa ya kusini iko nyuma kielimu,
naamini wa kusaidia kupandisha hadhi ni ninyi wenyewe mliosoma kule na wadau wengine
wanaoguswa na suala hili. “Msikate tamaa, mtafanikiwa. Cha msingi ni kuwashirikisha na
kuwashawishi wengine waliosoma ana kuwa karibu na mazingira ya kielimu ya mikoa hii.
Nchi hujengwa na wananchi wenye moyo, nanyi kwa kuguswa kwenu, naamini elimu ya
kusini itainuka kwa sababu ni vigumu mtu mmoja mmoja kuchangia na bado maendeleo ya
kweli yakaonekana, bali kupitia mshikamano kama wenu,” alisema mbunge huyo. Naye
Mratibu wa tamasha hilo, Asanterabbi Mtaki, licha ya kumshukuru mbunge huyo kwa nasaha
zake, aliwataka wadau wa elimu nchini kuungana na waliosoma mikoa ya kusini ili k
ufanikisha azma ya kuiinua kusini kielimu. “Tangu awali tumeelezea hali ya elimu ya mikoa
ya Kusini, kwa kweli si nzuri na inahitajika nguvu ya ziada, ndiyo maana tumeungana
kuhakikisha tunafanikisha kitu kwa ajili ya shule za kusini na wanafunzi wake, hasa yatima,
walemavu na wasiojiweza ili wapate haki ya kupata elimu bora,” alisema Mtaki. Alisisitiza
kuwa, kasi ya maandalizi ya tamasha hilo inaridhisha na kuongeza kuwa, nafasi ya waliosoma
kusini kuchangia mawazo bado ipo, hasa kupitia vikao vya kila mwisho wa wiki
vinavyofanyika ukumbi wa Imasco.
No comments:
Post a Comment