Monday, August 22, 2011

Naibu Waziri atoa changamoto ya elimu Lindi


Mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa, amewataka wakazi wa jimbo hilo kujifunga mikanda na kutenga fedha za kulipia ada za shule kwa watoto wao wa sekondari ili kuzalisha wasomi watakaosaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi. Aidha, Majaliwa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Elimu, alisema uwezo wake kwa sasa ni kulipia ada wanafunzi 105 tu wanaofaulu kuanza kidato cha kwanza kutoka familia maskini kila mwaka ili kuwapunguzia mzigo walezi wao. Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE Jumapili, Majaliwa alisema katika mwaka wa kwanza kama mbunge wa jimbo hilo, ameshatumia zaidi ya Sh milioni10 kusomesha wanafunzi 105 kutoka familia fukara kuanza kidato cha kwanza kwa utaratibu wa wanafunzi watano kutoka katika kila kata 15 za jimbo hilo. Alisema mbali na wanafunzi hao, Majaliwa alisema amewalipia ada ya mwaka wa pili wanafunzi 51 kutoka jimboni kwake wanaosoma sekondari ya wasichana ya mkoa wa Lindi, inayojulikana kama Ilulu Sekondari.
"Pia nimefanikisha kuwalipia Sh.800,000 wanafunzi wawili kutoka Ruangwa wanaosoma vyuo vikuu na wengine watano wa sekondari kwa maombi maalum na kwamba fedha hizo zimetoka katika mshahara wangu," alisema Majaliwa.
 Hata hivyo, mbuge huyo alisema inashangaza kuona wazazi na walezi wa jimbo lake wameanza kutafsiri vibaya msaada wake kwa kudhani atakuwa akifanya hivyo kila mwaka kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne, jambo ambalo alisema haliwezekani. "Ninachotaka kukifanya kwa miaka yote mitano ya utumishi wangu kama mbunge wa Ruangwa ni kusaidia kwa kadri nitakavyoweza wanafunzi wanaonza kidato cha kwanza kutoka familia maskini ili kuwapa nafasi wazazi au walenzi kujiandaa kwa miaka ijayo," alisema. Alisema anachofanya yeye ni kuwajengea misingi ya awali ya elimu ngazi ya sekondari na kwamba wanalo jukumu la kuendeleza misingi hiyo ili baada ya miaka mitano ijayo, jimbo liwe na idadi kubwa ya wasomi kwani anaamini wilaya yenye watu walioelimika ni rahisi kubadili uchumi wake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment